Baada ya Marekani, EU nayo kupitia misaada ya nje

Dar es Salaam. Wataalamu wa Tanzania na wadau wa asasi za kiraia, wametoa mapendekezo ya njia za kudumisha ufadhili baada ya Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani kutangaza kupitia upya misaada yao.

Umoja wa Ulaya utapitia upya mpango wake wa misaada ya kigeni, wenye thamani ya mabilioni ya Euro ili kuoanisha mgawanyo wa fedha hizo kwa karibu zaidi na masilahi yake ya sera za kigeni, Bloomberg imeripoti.

Hatua ya EU inakuja baada ya mipango ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kuanza utekeleza wa hatua kama hiyo, ikilenga kupitia upya au kufuta Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

Wakati huohuo, Tume ya Ulaya inakabiliwa na changamoto za kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi kutokana na vita vya Ukraine na tofauti za mtazamo na sera mpya za Marekani.

Tume ya Ulaya itasitisha utoaji wa misaada ya kigeni na kuifanya kuwa ‘ya kulenga zaidi kwa washirika,’ kwa mujibu wa rasimu ya nyaraka zilizoripotiwa na Bloomberg.

EU inataka kurekebisha misaada yake ya kigeni ili kukidhi masilahi yake ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na nchi zenye mwelekeo sawa, kupata malighafi muhimu na kupunguza wimbi la wahamiaji.

Bajeti ya jumla ya EU, ambayo kwa kawaida ni takriban asilimia 1 ya Pato la Taifa la jumuiya hiyo, inazidiwa mzigo kutokana na mahitaji mengi, kuanzia mabadiliko ya kijani hadi ulinzi.

Katika wiki zijazo, Tume ya Ulaya itaeleza mawazo yake ya kuboresha bajeti yake ya miaka saba ijayo kuanzia 2028 hadi 2034, Bloomberg imesema.

Trump amekuwa akilenga USAID tangu siku zake za kwanza madarakani. Utawala wake umeagiza kusitishwa kwa miezi mitatu kwa karibu ufadhili wote wa maendeleo ya kimataifa, na unaripotiwa kupanga kuwafuta kazi wafanyakazi wengi wa shirika hilo duniani kote.

Ikulu ya Marekani imekuwa ikiishutumu USAID mara kwa mara kwa matumizi mabaya na udanganyifu, ingawa misaada ya kigeni inachukua asilimia moja tu ya bajeti ya shirikisho.

Mapema wiki hii, utawala huo uliiweka USAID chini ya udhibiti wa Wizara ya Mambo ya Nje. Mnamo Februari 7, 2025 wafanyakazi walionekana wakiondoa nembo ya USAID kutoka mbele ya makao makuu ya shirika hilo jijini Washington.

Tangu kuanza kwa uvamizi wa Russia kwa Ukraine Februari 2022, USAID imetoa msaada wa kibinadamu wa dola bilioni 2.6, msaada wa maendeleo wa dola bilioni 5 na zaidi ya dola bilioni 30 kwa ajili ya bajeti ya moja kwa moja ya Ukraine.

Misaada ya shirika hilo inasaidia kujenga upya shule baada ya mashambulizi ya Russia, kugharamia ujenzi wa mahandaki ya mabomu, kurekebisha miundombinu muhimu ya nishati, na kufadhili miradi ya asasi za kiraia.

Njia mbadala kwa NGOs za Tanzania

Wataalamu wa Tanzania na waendeshaji wa asasi za kiraia wamependekeza hatua mbalimbali ambazo mashirika haya yanaweza kuchukua ili kuendelea na shughuli zao na kujihakikishia uendelevu wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage, aliliambia The Citizen kuwa kampuni za Tanzania zinapaswa kufikiria kusaidia na kuwekeza katika asasi za kiraia na NGOs ili kuhakikisha zinadumu.

Serikali inapaswa kutenga bajeti ya maendeleo, kwa ajili ya asasi za kiraia ili ziweze kuendelea kuwepo, amesema;

“Ni wakati mwafaka na mwito kwa Serikali kutafuta fedha za ndani ili kusaidia miradi yake ya maendeleo badala ya kutegemea misaada, mikopo nafuu, na ufadhili wa nje,” amesema.

“Taasisi za kimataifa ambazo hazijabadilisha msimamo wao kuhusu kuondoa misaada zinapaswa pia kufikiria kutupa fedha taslimu badala yake, ili tuweze kuwekeza katika miradi endelevu na kufanikisha ustahimilivu wa muda mrefu,” ameongeza.

Mtaalamu wa mitaji ya biashara, Salim Awadh amesema; “Nimesema mara nyingi kwamba, ikiwa NGOs hazitabadilisha mfumo wao wa ufadhili, zitapotea moja baada ya nyingine. Kama nilivyosema mara nyingi, asilimia 96 ya NGOs nchini Tanzania si endelevu kifedha.”