Baada ya dozi ya Azam, Ligi Kuu kupigwa tena leo

Mshike mshike wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo ambapo michezo miwili itapigwa kwenye viwanja tofauti huku macho na masikio yakielekezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba kwa mechi kali kati ya wenyeji Kagera Sugar dhidi ya KenGold.

Jana Azam ikiwa kwenye Uwanja wa KMC Complex ilimaliza gundu la ushindi baada ya kuichapa KMC mabao 4-0 na kupata pointi tatu za kwanza msimu huu.

Azam iliana karamu ya mabao dakika ya 19 wakati Fei Toto alipomnyang’anya mpira beki wa KMC na kumpasia Idd Selemani ‘Nado’ aliyeukwamisha kwa kumpiga chenga kipa Fabien Mutombora bao hilo lilidumu hadi mapumziko, licha ya wenyeji kucharuka kwa kutaka kulisawazisha.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Azam kuongeza bao la pili dakika ya 55 kupitia kwa nahodha Lusajo Mwaikenda aliyemaliza kazi nzuri ya Fei Toto na dakika tano baadaye Nassor Saadun aliandika bao la tatu lililokuwa tamu kutokana na kuwapiga chenga mabeki watatu wa KMC sambamba na kipa Mutombora.

Wakati KMC akijiuliza, Fei Salum aliambaa pembeni mwa uwanja na kupiga krosi iliyookolewa vibaya na mabeki wa wenyeji kabla ya Chilambo kuusukumia wavuni  dakika ya 67.

Katika mechi za leo, mchezo Kagera Sugar dhidi ya KenGold utapigwa saa 1:00 usiku ingawa utatanguliwa na mechi ya mapema saa 10:00 jioni itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, ambapo wenyeji Tabora United watakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Fountain Gate.

Ubora wa mchezo kati ya Kagera na KenGold, unatokana na timu zote kutoshinda michezo yao waliyocheza hadi sasa msimu huu huku kama haitoshi wenyeji licha tu ya kutopata pointi tatu kwenye mechi zao nne ilizocheza ila haijafunga bao lolote, huku wapinzani wao wakifunga mabao mawili kwenye michezo mitatu.

Kagera inayofundishwa na Mganda, Paul Nkata huenda huu ukawa mchezo wake wa mwisho na timu hiyo ikiwa atashindwa kupata pointi tatu baada ya kuambulia vipigo vitatu na kutoka sare mmoja, jambo ambalo linaonyesha hana maisha marefu kikosini humo.

Timu hiyo ilianza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha bao 1-0, kutoka kwa Singida Black Stars, ikachapwa tena mabao 2-0, dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, ikafungwa 1-0 na Tabora United kisha kulazimishwa suluhu na JKT Tanzania mechi iliyopita.

Kwa upande wa KenGold kutoka jijini Mbeya ambayo ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kutwaa ubingwa wa Championship msimu uliopita, haijaonja pia ladha ya ushindi katika michezo yake mitatu iliyocheza na kujikuta ikichapwa yote.

KenGold ilianza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha mabao mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, ikachapwa tena 2-1 mbele ya Fountain Gate Septemba 11, 2024, kisha kupoteza kwa bao 1-0, na KMC, mechi yake ya mwisho Septemba 16, 2024.

Licha ya KenGold kutopata ushindi hadi sasa ila inamtegemea nyota mshambuliaji, Joshua Ibrahim ambaye amekuwa na kiwango bora msimu huu, akifunga mabao mawili akiwa na kikosi hicho ambacho amejiunga nacho akitokea Tusker FC ya Kenya.

Kwa upande wa Tabora United na Fountain Gate, timu zote zinakutana zikiwa na pointi saba zikiwa nafasi ya nne na ya tatu baada ya kucheza michezo minne kila mmoja wao, huku hadi sasa zikitofautiana kwa mabao yao ya kufunga na kufungwa tu.

Katika michezo hiyo minne Tabora United inayonolewa na Mkenya, Francis Kimanzi imeshinda miwili, sare mmoja na kupoteza pia mmoja kama ilivyokuwa pia kwa Fountain Gate inayofundishwa na mzawa, Mohamed Muya jambo linaloongeza msisimko zaidi, hivyo timu itakayozoa pointi tatu hapa itajiweka kwenye nafasi nzuri.

Fountain Gate inaingia katika mchezo huu ikimtegemea nyota wa kikosi hicho Seleman Mwalimu ambaye kwenye michezo minne aliyocheza amefunga mabao matatu huku kwa upande wa Tabora United ikiongozwa na Mkongomani, Heritier Makambo mwenye bao moja.

Singida Black Stars inayofundishwa na Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ndiyo inayoongoza Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo minne na kushinda yote ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na Mashujaa yenye pointi saba ila ikicheza michezo mitatu.

Hata hivyo, kumekuwa na uhaba mdogo wa mabao kwenye ligi msimu huu baada ya hadi sasa kufungwa mabao 43 tu, huku moja likiwa la kujifunga.

Wakizungumzia maandalizi ya michezo hiyo, kaimu Kocha Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe alisema, presha ni kubwa kwao ila anaamini watafanya vizuri huku Kocha wa Kagera Sugar, Paul Nsata akieleza changamoto kubwa kwao ni kwenye umaliziaji