Azizi Ki atoa ng’ombe 30 mahari ya Hamisa

Dar es Salaam. Hatimaye kiungo mshambuliaji ya Yanga, Stephane Azizi Ki amelipa mahari ya ng’ombe 30 kwa mwanamitindo Hamisa Mobetto.

Mahari hayo yametolewa leo Jumamosi, Februari 15, 2025 katika hafla iliyofanyika viwanja vya Gofu Lugalo, Dar es Salaam.

Mahari hiyo imekabidhiwa na Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, kwa niaba ya baba mzazi wa Aziz Ki, ambapo nyota huyo aliongozana na baadhi ya wachezaji wenzake wa Yanga.

Mastaa waliohudhuria ni Pacome Zouzoua, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Kibwana Shomari sambamba na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe.

Kwa upande wa Hamisa aliingia ukumbini na meneja wake Paul Mangoma huku warembo 15 wakitangulia mbele wakiwa wamevaa sare huku wakicheza.

Hamisa ameiambia Mwananchi Digital kuwa, anamshukuru Mungu kumpata mtu anayeona ndiye anamfaa katika maisha yake na tayari sasa ni mchumba rasmi wa mtu.

“Sasa hapa ndio nimefika kwa kuwa nimekutana na mtu mwenye mapenzi ya kweli kwangu. Pia nafsi zetu zimeendana, hapa namuomba Mungu anyooshe mambo yaende kama vile tulivyopanga,” amesema Hamisa.

Kwa upande wake, Azizi Ki amesema anaamini safari yake ya muda mrefu imefika kwa kuwa amempata mwanamke anayempenda na kwa upande wake taratibu zote za uchumba amemaliza, anasubiri ndoa watakayofunga hivi karibuni.