Aziz Ki, Yanga wametukumbusha kaburi la wapendanao

Aziz Ki, Yanga wametukumbusha kaburi la wapendanao

Ukienda kule Kaole, Bagamoyo mkoani Pwani kuna hadithi ya kaburi la wapendanao ambayo utakutana nao.

Ni wapenzi wawili mwanamke na mwanaume ambao mmoja akiwa hai alikubali kuzikwa na mwenzake kama ishara ya kuthamini upendo ambao walikuwa nao katika mahusiano nao.

Emu fikiria katika kizazi cha sasa, mtu akubali kuzikwa hai kwa ajili ya mwenzake aliyefariki kisa tu walikuwa wapenzi inawezekana kama walivyofanya wapendanao wawili kule Kaole miaka mingi iliyopita?

Wengi kwa sasa watajibu haiwezekani kwa vile suala la mapenzi kwa wengi hivi sasa limejaa sanaa, ulaghai na purukushani nyingi ambazo zinaondoa hisia za ndani ambazo zinaweza kumfanya mtu aweke rehani uhai wake kwa ajili ya mwingine.

Nimeikumbuka Hadithi ya kaburi la wapendanao baada ya Yanga kufikia makubaliano na klabu ya Wydad ya Morocco ya kuwauzia kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki ambaye ni raia wa Burkina Faso.

Mapenzi ya Yanga kwa Stephane Aziz Ki yameifanya ikubali kuumia kwa kumuuza ili tu kutimiza ndoto za nyota huyo wa zamani wa Asec Mimosas za kucheza fainali za Kombe la Dunia la Klabu baadaye mwezi ujao.

Aziz Ki na Yanga kila mmoja alimpenda mwenzake na ndio maana kila upande umewahi kufanya uamuzi wa kujiumiza tu ili kuufurahisha upande mwingine.

Mwaka uliopita, Stephane Aziz Ki angeweza kupata kiasi kikubwa cha fedha kutoka timu mbalimbali zenye misuli ya kiuchumi ambazo zilionyesha nia ya kumhitaji lakini aliamua kuongeza mkataba wa kubaki Yanga ambayo hapana shaka fedha iliyomuwekea mezani haikuwa kubwa kulinganisha na hizo alizowekewa nje.

Lakini Aziz Ki aliona kuwa kuondoka Yanga kwa wakati ule tena bure, angeiumiza klabu hiyo ambayo katika kipindi chote alichoitumikia ilimfanya kuwa staa wake na kijana wao pendwa.

Yanga nayo ingeweza kumkomalia Aziz Ki na kugoma kumuuza kwa vile ina mkataba naye lakini imeamua kurudisha thamani ya heshima na upendo ambao nyota huyo aliionyesha kwao tena kwa uaminifu mkubwa.

Zipo sababu ambazo zimefanya pendo la Yanga na Aziz Ki Stephane kuwa kubwa kiasi cha kukaribia kulingana na kile kilichotokea kwa wapendanao Kaole.

Aziz Ki ameipenda Yanga kwa vile imempa heshima na hela nyingi katika kipindi chote alichoichezea. Afrika ilimfahamu zaidi Aziz Ki kupitia Yanga na sio Asec Mimosas.

Mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na watu wengi tofauti walimuimba na kumtaja mara kwa mara Aziz Ki kwa sababu ya Yanga.

Kupitia Yanga alikuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu Bara huku pia akiwa mfungaji bora na kubwa zaidi, Yanga ilimpa fedha ambayo hakuwahi kuipata alipokuwa Asec Mimosas.

Unaachaje kuipenda timu ambayo inakufanya uheshimike barabarani, madukani na hata kwa viongozi wakubwa wa nchi?

Nilitaka kusahau pia kuwa maisha yake ya Yanga ndio yamemfanya Aziz Ki kuoa mwanamke ambaye wanaume wengi Tanzania wana ndoto ya kuwa naye kwenye mahusiano, Hamisa Mobeto.

Lakini kwa Yanga ilikuwa lazima wampende kupitiliza Stephane Aziz Ki.

Aliwapa raha ya kuwanyanyasa watani wao Simba tangu alipokuwa Asec Mimosas hadi alipokuja nchini kuwatumikia.

Kwa utamaduni wa soka letu, Kufunga bao moja kwenye Kariakoo Derby ni zaidi ya kufunga mabao 20 dhidi ya timu nyingine. Emmanuel Okwi aliifungia mabao mengi mubimu Simba lakini heshima yake alianza kuipata baada ya kuifunga Yanga, mifano iko mingi sasa.

Lakini ukiachana na kuifunga Simba, Aziz Ki Stephane alikuwa ni mchezaji aliyeamua mechi nyingi ngumu za Yanga mojawapo ni ile ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini dhidi ya Club Africain ya Tunisia ambayo alifunga bao pekee lililoivusha Yanga kuipeleka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 2018.

Stephane Aziz Ki anaondoka akiwa haidai Yanga wala timu hiyo haimdai kiungo huyo anayechezea timu ya taifa ya Burkina Faso.

Mapenzi yao hayakujificha kama yale ya wapendanao waliozikwa pamoja  Kaole Bagamoyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *