Aziz Ki kuivaa Man City, aacha rekodi

Kiungo wa Yanga Stephen Aziz Ki, juzi usiku aliondoka nchini kuelekea Morocco kujiunga na klabu ya Wydad Athletic ya nchini humo, huku akiacha rekodi kibao kwenye soka la Tanzania.

Ki alijiunga na Yanga akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coasta na ameshatumika kwenye Ligi Kuu kwa misimu mitatu akifanya mambo makubwa kwenye kikosi hicho.

Kiungo huyo ambaye ameondoka Yanga baada ya kuwindwa na timu kadhaa msimu uliopita, bado alikuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, baada ya kusaini miaka miwili mwishoni mwa msimu uliopita.

Kwa nini kaondoka mapema

Aziz Ki alilazimika kuondoka juzi ikiwa ni siku moja kabla timu yake mpya ya Wydad haijaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na michuano mipya ya Klabu Bingwa Dunia inayofanyika nchini Marekani kuanzia Juni 14  hadi Julai 13, 2025.

Hii ni michuano mipya ambapo Wydad ipo kundi G ikiwa pamoja na Manchester City ya England, Juventus ya Italia, Al Ain ya Saudia.

Kwa mara ya kwanza Ki anaweza kuwa uwanjani Juni 18 wakati timu hiyo itakapovaana na  Man City Juni 18, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Lincoln Financial Fied ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Kundi G.

Baada ya mechi hii, Aziz Ki ambaye amekuwa akionyesha kiwango cha juu uwanjani, atarudi tena uwanjani Juni 22 kuvaana na Juventus, baada ya hapo atamaliza mechi za makundi Juni 26, wakati timu hiyo itakapovaana na Al Ain.

Haya ni mashindano mapya ambapo kwa Afrika yanashirikisha timu za Al Ahly, Esperance de Tunis, Mamelodi Sundowns na Wydad.

Akiwa kwenye kikosi cha Wydad atakutana na mshambuliaji wa zamani wa Fountain Gate mzawa, Seleman Mwalimu, ambaye amekuwa akionyesha kiwango cha juu na aliondoka nchini akiwa amefunga mabao sita kwenye Ligi Kuu Bara.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Wydad kuvaana na Man City pamoja na Juventus ya Italia kwenye mechi ya mashindano.

Makombe sita

Aziz Ki ameondoka Yanga akiwa ameacha mambo mengi ya kukumbukwa, lakini kubwa kuliko yote ni uwezo wake uwanjani na kiwango ambacho alikuwa akikionyesha kwenye kila mchezo aliopata nafasi.

Akiwa na Yanga kwa misimu mitatu, kiungo huyo ambaye ni mume halali wa Mtanzania Hamisa Mobetto, amefanikiwa kutwaa makombe yote makubwa ya ndani.

Ametwaa Ligi Kuu Bara mara mbili, (ukiachana na msimu huu), Kombe la FA mara mbili, Ngao ya Jamii mara mbili, Kombe la Muungano mara moja pamoja na kuiongoza Yanga kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo.

Pia kiungo huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto, mwenye uwezo wa juu wa kufunga kwa mikwaju ya kutenga, alikuwa mmoja wa wachezaji walioiongoza Yanga kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25, kwenye historia ya klabu hiyo.

Mabao, pasi kibao

Kiwango cha Aziz Ki kwenye Ligi Kuu Bara kimekuwa bora kwa kipindi chote ambacho akiwa ana tuzo moja ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambapo alifanikiwa kufunga mabao 21.

Jumla staa huyo raia wa Burkina Faso amefanikiwa kufunga mabao 46 kwa kipindi alichokaa Yanga, amefunga mabao 39 kwenye Ligi Kuu Bara, Kombe la FA manne (msimu huu), Ligi ya Mabingwa moja na Kombe la Shirikisho Afrika mabao mawili.

Mbali na mabao, kiungo huyo ana rekodi ya kutoa pasi 18 kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa kipindi chote alichokaa hapa nchini, Aziz Ki amefunga ‘hat trick’ mara tano, akifunga nne kwenye Ligi Kuu Bara na moja kwenye michuano ya FA.

Kiungo huyo ni mmoja kati ya wachezaji ambao wamefanikiwa kuifunga Simba mabao mengi baada ya kufanikiwa kufanya hivyo mara tatu kwenye kipindi chote walichokutana.

Ki anakumbukwa kwa bao alilofunga kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi ambalo mwamuzi alilikataa pamoja na mpira kuonekana kuwa ulivuka mstari.

Ratiba ya Wydad Klabu Bingwa Dunia

Juni 18. Manchester City vs Wydad AC

Juni 22. Juventus vs Wydad AC

Juni 26. Wydad AC vs Al Ain

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *