Dar es Salaam. Hata sijui walipangaje miadi yao. Lakini walikutana kule bustanini wakapiga stori flani, yeye na nyoka. Baadaye akarudi kumjaza ujinga huo Adam. Na kwa pamoja wakala kikatili lile tunda la mti wa katikati.
Kila kitu kikabadilika kuanzia hapo. Mishe mishe zikawa ngumu kwa masela. Msako wa pesa ukawa wa jasho na damu. Hata pisi kali nazo, zikaanza kujifungua kwa uchungu. Kisa Eva a.k.a Hawa huyo!
Kuna pisi iliyozimiwa na mwamba. Samsoni jitu la mtumba. Pandikizi la mtu. Miraba minne lenye uwezo wa kupigana na jeshi la nchi yote. Likatoa boko kijinga, siri za nguvu zake zikagundulika. Kisa Delila.

Stori za hawa mademu maarufu zaidi duniani. Usisome kwa hisia hasi bali kwa hisia chanya. Ujue wana nguvu kubwa. Leo usishangae wao kuiendesha dunia. Ndiyo waliofanya dunia iwe hivi.
Ukifanya kinachohusu mwanamke, lazima kiwe kikubwa. Muziki ni dili kubwa, kwa sababu yao. Muziki ni mali yao. Ni wanunuzi wa kazi za muziki na wahudhuriaji sana wa matamasha ya muziki.
Wanaume tunakwenda kwenye matamasha kwa sababu yao. Kama siyo ushawishi wa kuwakatia tiketi, basi kuwatazama ukumbini. Mtoto flani unakuta kapendeza akicheza muziki. Mzuri kuliko wimbo!
Masela wanabebana kibao kwenda kwa shoo ya Jay Melody au Marioo. Siyo kufuata muziki wake, bali kwa kuamini kutakuwa na totozi kibao. Wanaume wanaenda kufuata pisi.
Lakini ni ngumu Tina na Edna kama siyo Asha. Kwenda kwenye shoo ya Mbosso, eti kwa sababu kutakuwa ya mabishoo. Wao hufuata muziki na Mbosso tu. Hapa kuna tofauti kubwa sana.
Filamu ni biashara inayomgusa mwanamke. Wao hupenda simulizi na maongezi. Muvi itamchekesha, kumuumiza au kumkera. Wao wana hisia kali kuliko wanaume. Masela hisia ‘hatunaga’.

Wenye akili zao. Wakiwa ndani ya jengo maridadi juu ya vilima pale Zurich Uswizi. Makao Makuu ya soka yaani FIFA. Wakaliona hili. Na wao kwa pamoja wakaamua soka kulikabidhi katika mioyo ya kike.
Soka ni pesa nyingi. Lakini muziki na filamu ni zaidi. Kwa sababu ya kufunga ndoa na mioyo yao. Fifa wameamua. Soka linaingizwa kwenye nyoyo za wanawake. Kulifuatilia au kuingiza viashiria hivyo.
Kamera kuelekezwa zilipo pisi kali viwanjani siyo bahati mbaya. Hata viongozi wa kike kujazana kwenye taasisi za soka siyo bahati mbaya. Ni oparesheni kuijaza biashara ya soka kwenye mioyo ya kike.
Fifa wako ‘siriazi’ na suala hili. Ndiyo maana ni lazima kila klabu kuwa na timu ya wanawake. Hilo hatuwezi kuona matokeo yake hivi karibuni. Kwa sababu ngozi nyeupe hufanya mipango ya miaka 50 mbele.
Tunaweza tusiwepo nyakati hizo. Kipindi soka litatii na kuishi kwao. Kama ilivyo kwenye filamu, muziki na tamthilia na simulizi. Kuna ‘taim’ sebule zitajaa kina mama uswazi wa kitazama soka kama tamthiliya.
Baada ya Mungu ni Mzungu. Kama wakati wa dunia ya gizani. Weupe waliweza kueneza na kutujaza sisi tamaduni zao. Washindwe kuijaza biashara ya soka kwenye mioyo ya mama zetu? Leo?
Bahati nzuri kina mama nao wana mioyo rahisi sana. Wanaamini kwa kasi kuliko ‘esijiara’. Mpaka sasa muitikio wa kina mama kwenye dili la soka unavutia. Tunaona jukwaani na kwenye pombe.
Wanunuzi na wavaaji wakubwa wa jezi ni wao. Zunguka kitaa tazama pisi kali na uzi za kina Pacome. Ni muda mfupi ujao soka litakuwa ni biashara kubwa zaidi kwa dunia hii. Hili halibishiwi.
Kuna ‘taimu’ mtu anasogea pale Kwa Mkapa. Siyo kwa sababu ya kina Chasambi na Mukwala. Ni vile wanaona picha mitandaoni za pisi zikijiachia majukwaani pale Taifani kwa Mkapa. Noma!
Kuna ‘taimu’ jukwaa tamu zaidi ya katikati ya dimba. Naangaliaje pasi ya Kibu, wakati mbele yangu kuna Hamisa anakatiza? Tuwe ‘siriazi’ na maisha bro. Soka nimetazama toka enzi za Said Mwamba Kizota.

Leo hii inawezekana kuna bwege tu. Eti anakerwa na uwepo wa Misa kando ya Aziz Ki. Lakini amini hivi, wenye soka lao pale Zurich hilo ni bao. Wanatamani Pacome na yeye ajiweke hata kwa Gigy Money.
Huu ni ushindi kwa FIFA na dili lao la soka kwenye nyoyo za wanawake. Ni wazi kwamba Aziz Ki ‘ana asisti’ nje ndani. Nje na ndani ya uwanja kwa kulipeleka soka kwa mamajusi wa karne ya 21.
Sikiliza we ndezi unayekatika stimu na Aziz na Misa. Muziki wa Hip Hop, mwanzo ulipendwa na wahuni, Masela, Majita na masimela. Lakini kibiashara haukuwa na namba nzuri. Hii ni Marekani na Bongo.
Lakini baada ya kuzama kwenye mioyo ya wanawake. Kuanza kuhusudiwa na kina Delila na Eva. Ukatuumbia mamilionea wapya kupitia muziki huu na kuuza kopi nyingi. Amini nakwambia, mwanamke ni noma.
Wanawake ni jeshi kubwa sana. ‘Hepi Wumeni Dei Ini Advansi’