Dar es Salaam. Yametimia. Ni kweli, ndizo kauli za wengi baada ya kushuhudia mwanamitindo Hamisa Mobetto na mchezaji wa Klabu ya Yanga, raia wa Burkina Faso, Aziz Ki wakivishana pete ya uchumba na kuhitimisha minong’ono ya muda mrefu.
Awali, yalikuwapo mawazo mchanganyiko ndani ya jamii kuhusu wawili hao, baadhi wakiamini kilichokuwa kikifanyika ni maandalizi ya filamu au matangazo ya biashara.
Kitendo cha wawili hao kuweka hadharani uchumba wao leo Februari 15, 2025 wakitarajiwa kufunga ndoa Februari 16, kinamaliza uvumi uliodumu kwa takribani miezi minane tangu wawili hao waonekane kwa mara ya kwanza wakiwa pamoja Mei 20, 2024.

Aziz Ki akiwa amepiga goti, alimuomba Hamisa kukubali ombi la kuwa mkewe, muda mfupi baada ya kukamilisha taratibu za utoaji mahari.
Tukio hilo limefanyika katika viwanja vya Golf Club, Lugalo jijini Dar es Salaam.
Tukio la Hamisa kuvishwa pete limeshuhudiwa na wanafamilia na watu wa karibu na kuweka rasmi uhusiano wao, ambao licha ya kuwekwa hadharani kwa takribani wiki moja iliyopita, ulionekana ni mzaha.

Baada ya wanafamilia wa Hamisa na wageni wengine kuwasili, ilifuata familia ya Aziz Ki ikiongozwa na rais wa Yanga, Hersi Said aliyesimama nafasi ya baba mlezi wa mchezaji huyo.
Hersi ndiye aliyekabidhi mahari kwa niaba ya familia.
Muda ulipowadia, Aziz Ki aliingia katika eneo hilo akiwa ameambatana na baadhi ya wachezaji wenzake wa Yanga na maofisa wa kitengo cha habari cha klabu hiyo, wakiongozwa na msemaji wa klabu, Ali Kamwe.

Dakika chache baadaye, aliingia Hamisa na moja kwa moja kumtambua mume wake mtarajiwa, hivyo kutoa ruhusa kwa familia yake kupokea mahari.
“Tumekuita hapa mwanaume huyu na familia yake wamekuja kutoa mahari, sasa tunakuuliza ndiye yeye na kama ndiye uturuhusu tupokee mahari,” alisikia mmoja wa ndugu wa Hamisa akimhoji mwanamitindo huyo.
Hamisa alikiri kumtambua mwanamume huyo na kuridhia familia ipokee mahari ambayo pamoja na vitu vingine walikuwepo ng’ombe 30 na jukumu la kukabidhi lilikuwa la Hersi.
Baada ya kukamilika taratibu za kutoa mahari, Aziz Ki alimvalisha Hamisa pete ya uchumba na kuzima uvumi kwamba wawili hao hawapo kwenye biashara, kama ambavyo ilikuwa ikifikiriwa na wengi.

Kutoaminika kwa tukio hilo awali kulitokana na historia ya Hamisa ambaye mara kadhaa amekuwa akihusishwa na wanaume ambao baadaye hubainika walikuwa wakifanya biashara na si uhusiano wa kimapenzi.
Mfano wa hilo ni kile kilichotokea akiwa na ukaribu na rapa wa Marekani, Rick Ross, wengi wakiamini wana uhusiano wa kimapenzi.
Baada ya muda ikawekwa wazi kuwa msanii huyo alimtumia Hamisa kama balozi wa kinywaji chake.
Hamisa, mama wa watoto wawili pia aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Nassib Abdul maarufu Diamond Platnumz, Mkurugenzi wa EFM Francis Ciza (Majay) na kila mmoja amezaa naye mtoto mmoja.
Kuhusu uhusiano wake na Aziz Ki, licha ya wenyewe kudai ulikuwepo kwa muda mrefu, umeonekana kushika kasi ndani ya juma moja walilotangaza tarehe ya mahari, ndoa na sherehe ya kuwapongeza.
Februari 14 siku ya wapendanao kupitia ukurasa wake Instagram, Aziz Ki aliandika: “Kama mchezaji wa mpira wa miguu, maisha yangu yanaundwa na maamuzi makubwa kuhama, kupiga mashuti na chaguo zinazoelekeza safari yangu, lakini uamuzi mmoja ambao sijawahi kuutilia shaka, hata kwa sekunde moja ni kukuchagua wewe.

“Tangu nilipokutana na wewe, nilijua kuwa wewe ni wa milele kwangu pamoja na wewe, hakuna kuanguka ni kupaa tu, wewe ni ushindi wangu mkubwa zaidi, ndoto yangu nzuri zaidi iliyotimia. Mwaka jana, nilichukua shuti muhimu zaidi siyo uwanjani, bali nikiwa nimepiga goti moja chini na uliposema ndiyo, dunia yangu ilibadilika milele. Nakupenda sana, Hamisa asante kwa kunichagua, kwa kunipenda na kwa kutembea nami kwenye safari hii.”
Hamisa alijibu: “Mpenzi wangu, wewe ni baraka yangu kubwa zaidi, kimbilio langu salama na milele yangu. Kukuchagua wewe ilikuwa uamuzi rahisi zaidi niliowahi kufanya, kwa sababu moyo wangu ulijua daima ilikuwa wewe. Kila muda nilio na wewe ni ndoto na siwezi kusubiri milele yetu ifunguke. Nakupenda zaidi, mfalme wangu. Asante kwa kunipenda jinsi unavyonipenda.”
Safari yao
Kwa mara ya kwanza wawili hawa walionekana pamoja Mei 20, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Hamisa akiwa katikati ya kundi la wachezaji wa Yanga waliotua uwanjani hapo.

Hata hivyo, Aziz Ki pekee ndiye aliyekuwa akizungumza na Hamisa ambaye alionekana kuwa na wasiwasi kidogo na kuanzia hapo uvumi wa wawili hao kuwa pamoja ulianza.
Juni 10, 2024 akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari, Hamisa aliulizwa kuhusu ukaribu wake na Aziz Ki, alikana kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi lakini akaweka wazi kuwa ni rafiki yake.
Baada ya hapo haikuwa kitu cha ajabu kwa Hamisa kuonekana uwanjani wakati Yanga ikicheza na mara zote alikuwa karibu na Aziz Ki hata kufikia hatua ya kumsindikiza kupokea tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Hata wakati wa Wiki ya Wananchi Agosti 4, 2024, Hamisa alipanda jukwaani wakati Aziz Ki anatambulishwa, kisha mwanasoka huyo akamvalisha jezi ya Yanga.
Februari 9, 2025 ndipo wawili hawa walipovunja ukimya na kuutangazia umma kuwa wanatarajia kufunga ndoa wakiwa wameweka mtandaoni ratiba ya shughuli tatu ambazo ni mahari, ndoa inayofungwa Februari 16 na sherehe ya kuwapongeza itakayofanyika Februari 19.