Dar es Salaam. Habari ya mjini ni ndoa ya nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki na Hamisa Mobetto, kila mmoja akisema lake, huku kiungo mshambuliaji huyo wa Yanga akithibitisha kile ambacho kilizungumzwa kwa siku kadhaa kwa kufunga ndoa na mrembo huyo.
Aziz Ki na Mobetto wamefunga ndoa katika moja ya msikiti huko Mbweni jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Februari 16, 2025, tukio lililotanguliwa na mahari jana Jumamosi, Februari 15, 2025.
Ndoa hiyo, ambayo unaweza kusema ‘ndo habari ya mjini’ kutokana na kujadiliwa na kufuatiliwa maeneo mbalimbali, si ya kwanza kwa mastaa kuoa Tanzania, huku mchambuzi wa masuala ya mahusiano akitaja mambo manne yanayosababisha ndoa za aina hiyo.
Ndoa hiyo iliyofungwa Mbweni, ilishuhudiwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar, akiambatana na Aziz Ki kumfunua bibi harusi, Mobetto, baada ya kutoka msikitini.

Sheikh Walid alimsindikiza bwana harusi kisha kumsomea dua, kumshika kichwa, kabla ya Aziz Ki kumfunua bibi harusi katika tukio hilo la ndoa yao iliyokuwa gumzo nchini ikirushwa mubashara.
Siku moja kabla ya ndoa, Mobetto alilipiwa mahari ya ng’ombe 30 na fedha taslimu Sh30 milioni, mahari iliyokabidhiwa na rais wa Yanga, Hersi Said, kwa niaba ya baba mzazi na wajomba wa Aziz Ki, ambao ni raia wa Burkina Faso.
Ndoa ya Aziz Ki na Mobetto imehudhuriwa na mastaa mbalimbali, wakiwepo wachezaji wa Yanga, ambao wamesimama kama ndugu wa bwana harusi kwa Tanzania.
Baada ya sherehe ya ndoa leo, inaelezwa kwamba Februari 19, 2025 kutakuwa na sherehe nyingine kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Mastaa wengine
Ndoa ya Aziz Ki ni muendelezo wa mastaa wengine waliowahi kuoa Tanzania na ndoa zao kuwa gumzo, akiwemo mchezaji kutoka Rwanda, Hamad Ndikumana (sasa ni marehemu).
Ndikumana alikuwa gumzo alipofunga ndoa na mrembo Irene Uwoya mwaka 2008 na kubahatika kupata mtoto mmoja.
Felix Sunzu, raia wa Zambia, nyota wa zamani wa Simba, naye yumo kwenye orodha hiyo baada ya kufunga ndoa na Juliana Enock kutoka Mwanza.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa Simba msimu wa 2011/12, mpaka sasa anaishi na mkewe jijini Mwanza, wakiwa wamebahatika kupata watoto watatu.
Juni 2023, katika mahojiano na gazeti dada la Mwananchi, Mwanaspoti, Sunzu alisema amechagua kuishi Tanzania kwa kuwa watu wake ni wakarimu.
“Nimeoa Tanzania na nina watoto watatu hapa, nilikuwa na familia tangu nachezea Simba, huwa nakwenda nyumbani Zambia kusalimia, kisha narudi tena,” alisema Sunzu.
Alisema maisha ya Tanzania ni mazuri sana, anapenda vyakula vya Kitanzania hasa wali, maharage, na kuku, huku Tanzania watu wanavaa wanavyopenda na huwa hatamani kwenda popote kwa kuwa hapa Tanzania amefika.
Mwenyeji mwingine ni Mnigeria, Abaslim Chidiebele, aliyewahi kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na timu za Stand United ya Shinyanga na Coastal Union ya Tanga kwa nyakati tofauti, naye ameoa Mtanzania na anaishi Shinyanga.
Mchezaji huyo alikuja nchini mwaka 2012, mbali na timu hizo, pia amewahi kucheza Pamba ya Mwanza ikiwa ligi daraja la kwanza na Mbeya City.
Mbali na wanasoka, mwanamuziki Boniface Kikumbi maarufu King Kiki (sasa ni marehemu) pia alioa Mtanzania, Constasia Kalanda, na alipata nao watoto kadhaa.
Mwanamuziki huyo aliyeimba wimbo wa Kitambaa Cheupe alizaliwa mwaka 1947 katika jiji la Lubumbashi, DR Congo.
‘Mambo manne’
Akizungumzia sababu za watu kuamua kutoka nchini kwao na kuoa au kuolewa na watu wa nchi nyingine, mwanasaikolojia na mchambuzi wa masuala ya mahusiano kutoka Taasisi ya Wezesha Jamii, Deogratius Sukambi, amesema zipo nyingi.
Amesema sababu ya kwanza katika muktadha wa saikolojia ni mtu kuona anafaa, hivyo kuwa na kiu ya kutaka kuendana na jamii anayoishi nayo, hasa pale anapokubalika.
“Ule msukumo unakusukuma kuanzisha commitment hiyo,” amesema.
Amesema jambo la pili ni utamaduni wa jamii hiyo aliyopo.
“Unapokutana na utamaduni wa jamii nyingine tofauti na yako, ukakuvutia, huwa inatokea, hivi, na hapa ni ule utamaduni wa mwanaume kumhudumia mwanamke au mwanamke kumhudumia mwanaume,” amesema.
Amesema kila jamii ina namna yake ya kuhudumiana, hivyo mtu anapokutana na kitu kipya kikamvutia inasababisha jambo hilo.
“Jambo la tatu huwa wapo watu wanaokimbia kelele za jamii aliyopo, mwingine anaona tayari alishakuwa staa, mambo yake yanajulikana kwa mashabiki, vitu ni vingi, hivyo anataka kuanza upya maisha yake,” amesema Sukambi.
“Mtu huyu utakuta amejitafuta na kujipata, atataka kuoa nje ya jamii yake, hata hapa Watanzania wapo wasanii wakubwa au mastaa wanakwenda kuoa nje ya nchi, watu wanajiuliza, kwani huku kwao hawapo wanawake au wanaume? Ila yeye ataona bora akaoe au kuolewa kwingine,” amesema.
Amesema jambo la nne ni uhusiano wa jamii husika inayomzunguka. Wapo wengine huwa wanaanzisha mahusiano kujaribu, lakini watu wanaomzunguka watachochea na kuona kumbe inawezekana kuoa.
“Hizi ndoa zinahitaji muda kuona muendelezo wake baadaye, kama ilikuwa ni yeye au watu waliomzunguka walimchochea, kama ilikuwa ni yeye zinadumu, na kama kinyume zinaishia njiani,” amesema.