Aziz KI aingia anga za MO Salah, Mane

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Aziz KI anawania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka kwenye tuzo za African Golden Awards akishindana na nyota kibao wa Afrika wakiwamo Mohamed Salah wa Liverpool na Sadio Mane wa Al Nassr.

Aziz KI, nyota huyo wa kimataifa wa Burkina Faso anawania kipengele cha pili kwenye tuzo hizo zitakazotolewa Aprili 5, mwaka huu, nchini Kenya awali akiwania kwenye ‘kapo’ bora ya mwaka ambayo yupo na mkewe mwanamitindo Hamisa Mobetto.

Mchezaji huyo anayekipiga Ligi Kuu Bara anaingia kwenye kipengele hicho kinachowaniwa na wachezaji 16 kutoka Afrika wanaokipiga katika ligi mbalimbali duniani.

Ukiachana na Mane na Salah wanaowania tuzo hiyo wengine ni Riyad Mahrez ( Al-Ahli ), Ademola Lookman (Atalanta), Kalidou Koulibaly (Al-Hilal), Amad Diallo (Man United), Achraf Hakimi (PSG), Thomas Partey (Arsenal), Andre Onana (Man United).

Wapi pia kina Franck Kessie (Al-Ahli), Michael Olunga(Al-Duhail), Ronwen Williams (Mamelodi Sundown) na Mohamed Kudus (West Ham United).

Huu ni msimu wa tatu kwa nyota huyo Mburkinabe kuichezea Yanga akisajiliwa kutokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Msimu wake wa kwanza kwenye mechi nane alifunga mabao tisa ilhali uliofuatia aliibuka mfungaji bora akitupia kambani mabao 21 na msimu huu tayari amefunga saba katika mechi 22.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *