Aziz KI ahesabu siku Yanga

SUALA la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI kuendelea kuwapo ndani ya kikosi hicho ni jambo la muda tu kuanzia sasa kutokana na matajiri wa Kiarabu kujipanga kumng’oa Jangwani.

Aziz Ki anayemiliki mabao saba na asisti saba katika Ligi Kuu msimu huu inaelezwa anamenyemelewa na klabu mbili kubwa kutoka Morocco zilizoanza mazungumzo na mabosi wa Yanga ili kumnunua kwa msimu ujao, huku mabosi hao wa Jangwani wakiwa tayari wameshapiga hesabu za mbadala wa kiungo huyo.

Kiungo huyo raia wa Burkina Faso, anaitumikia Yanga kwa sasa kwa msimu wa tatu tangu alipotua akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast akiwa ndiye alikuwa Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga mabao 21.

Katika msimu wa kwanza Aziz Ki alicheza na Fei Toto alimaliza na mabao tisa chini ya kocha Nasreddine Nabi aliyeondoka kumpisha Miguel Gamondi na msimu uliopita mambo yalimnyookea akifunga mabao 21 yaliyoiwezesha Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo.

Iko hivi. Aziz KI aliongeza mkataba wa miaka miwili na kwa sasa anamaliza mwaka wa kwanza, hivyo timu inayomhitaji inatakiwa kumnunua kwa bei ambayo Yanga itaihitaji.

Kilichowavutia zaidi Waarabu hao ni rekodi za kiungo huyo, hasa za msimu uliopita aliwapowafunika nyota wote wa Ligi Kuu kwani licha ya kufunga mabao 21, pia aliasisti mabao manane, huku msimu huu akiwa amehusika katika mabao 14 hadi sasa.

Mwanaspoti linafahamu, hadi sasa klabu mbili ndizo zilizogonga hodi kwa Yanga, ikiwamo FAR Rabat na Raja Casablanca zote kutokea Morocco.

Taarifa hizi zinaeleza kwamba mabosi wa Jangwani wameanza mazungumzo na FAR Rabat, juu ya hatua ya kumuuza mwisho wa msimu, huku pia mabingwa wa Morocco, Raja nao wakielezwa wanajaribu kumsaka kiungo huyo, hivyo mwenye kisu kikali ndiye atakayekula nyama.

Kuna uwezekano mkubwa dili hilo likamalizwa na FAR Rabat, kwa kuwa tayari wameshafikia hatua nzuri ya kumaliza dili hilo na kama atatimkia huko atakutana na beki Henock Inonga aliyekuwa akiitumikia Simba kabla ya kutimka Morocco msimu huu.

Katika Ligi Kuu ya Morocco (Batola Pro), FAR Rabat iliyokuwa chini ya kocha Nabi msimu uliopita, inashika nafasi ya pili ikiongozwa na RS Berkane, huku Raja ikishika namba nane kwa sasa wakiwa pia ndio watetezi wa taji waliolitwaa kwa kuzidi ujanja maafande wa FAR Rabat dakika za lala salama.

KIGOGO ATUA MOROCCO

Taarifa za ndani ziliiambia Mwanaspoti kuwa, kabla ya mechi ya juzi usiku iliyopigwa Azam Complex, kati ya Yanga na Azam FC, ambapo wenyeji walipasuka kwa mabao 2-1, mmoja wa viongozi wa juu wa klabu ya Jangwani, alikuwa Morocco.

“Hakuna anayejua alienda huko kwa sababu zipi ili huenda akawa ameenda kwenye mazungumzo ya kumuuza kiungo huyo, kwani tayari kuna mazungumzo yalishaanza na bahati nzuri klabu zote zinazotajwa kumtajka Aziz Ki zipo nchini humo,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kilichoeleza uwepo wa Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said huko Morocco kabla ya kuiwahi mechi ya juzi.

Sasa inaelezwa, kwa namna dili ya Aziz Ki lilipofikia mabosi wa Yanga wameanza mipango ya kumrejesha Feisal Salum kutoka Azam.

FEI NI HIVI

Ukirudi msimu miwili nyuma, utakumbuka Fei Toto (anayekipiga Azam FC kwa sasa) alicheza pamoja na Aziz KI katika kikosi hicho kwa nafasi moja ya namba 10, huku Fei akimkalisha mara kadhaa benchi nyota mwenzake kabla ya kuanzisha mgomo uliompeleka kwa Matajiri wa Chamazi.

Sasa inaelezwa kuwa, kwa namna dili ya Aziz Ki lilipofikia mabosi wa Yanga wameanza mipango ya kumrejesha Fei Toto, japo kiungo anayemiliki mabao manne na asisti 13 kwa sasa akiwa na Azam anawindwa pia na Simba akielezwa anayeendana na soka la Msimbazi.

Kwa sasa Fei Toto ana mkataba wa mwaka mmoja na ushei na klabu ya Azam ilishaweka wazi kwa atakayetaka saini yake, basi aende mezani akiwa na Sh1 bilioni ili kumpata.

Hata hivyo, Yanga imekuwa ikimpigie hesabu kwa kuona kama ndiye mtu anayeweza kuziba nafasi ya Aziz KI kama dili la Morocco litatiki, ingawa mchezaji huyo Mzanzibari aliwahi kunukuliwa kwamba anatamani kucheza soka la kulipwa na awali alikuwa akiwindwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Kaizer imekuwa ikimwinda Fei Toto tangu mapema msimu huu, lakini ilishindwa kufikia dau lililowekwa na klabu ya Azam ya Dola 500,000 (zaidi ya Sh1.3 bilioni) kwani walipeleka mezani Dola 300,000 kabla ya kuongeza nyingine 50,000 na kuwa Dola 350,000 ambazo zote zilikataliwa katika dirisha dogo lililofungwa Januari mwaka huu.

“Kaizer imeshaifuata Azam rasmi kwa ajili ya mazungumzo ya kumpata kiungo huyo msimu ujao ikiwa tayari kufikia dau la matajiri hao wa Chamazi, lakini ilishindikana,” chanzo kutoka Azam kiliweka bayana kilipozungumza na Mwanaspoti, japo kilidokeza Simba na Yanga hazijaenda mezani kwao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *