STEPHANIE Aziz KI ameshatimka rasmi nchini baada ya Yanga kufikia makubaliano ya kumuuza katika klabu ya Wydad Athletic ya Morocco ambayo anaenda nayo kuzivaa Manchester City na Juventus katika Kombe la Dunia la Klabu mwezi ujao huko Marekani.
Kuondoka kwa Azizi KI kunahitimisha msimu mitatu ya kiungo huyo aliyesajiliwa na Yanga akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Kuna mambo mazito Aziz KI ameyafanya akiwa na Yanga ndani ya misimu mitatu ambayo sio rahisi kusahaulika mpaka anapoondoka ndani ya klabu hiyo bingwa wa muda wote nchini Tanzania na zifuatazo ni alama tano zilizoachwa Yanga na kiungo mshambuliaji huyo wakati akienda Wydad.
MABAO 54, ASISTI 32
Aziz Ki anaondoka Yanga akiwa na heshima kubwa ya kuhusika katika mabao 86 kwenye mechi 114 za michuano yote, akifunga mabao 54 na kutoa asisti 32, huku kati ya hayo mabao 39 ni ya Ligi Kuu, yakiwamo 21 yaliyompa tuzo ya Mfungaji Bora msimu uliopita akimzidi Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyemaliza na mabao 19.
Kwa msimu huu pekee ameondoka akiwa amefunga mabao tisa na asisti saba katika Ligi Kuu, huku Kombe la Shirikisho (FA) akiwa na mabao manne wakati akipiga hat trick dhidi ya Stand United, na katika michuano ya CAF ambako Yanga ilitolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga manne yakiwamo mawili ya hatua ya makundi.

MAKOMBE TISA
Ndani ya misimu mitatu Aziz KI amepata makombe tisa akiwa na kikosi hicho yakiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, mengine mawili ya Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii mbili, Kombe la Muungano, Toyota na Mapinduzi yote akichukua moja katika kila shindano.
Mbali na mataji hayo, Aziz KI ameondoka nchini akiwa amebeba tuzo mbili za maana kubwa, ikiwamo ya Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa msimu uliopita, hapo ni mbali na zile za Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu zinazotolewa mara kadhaa.
Tuzo ya Mchezaji Bora kwa Aziz Ki ni muendelezo wa rekodi aliyowahi kuiweka wakati akiwa Asec Mimosas ya Ivory Coast kabla ya kusajiliwa na Yanga chini ya kocha Nasreddine Nabi.
HAT TRICK TANO
Hadi anaondoka Yanga, Aziz KI amejipambanua ni mchezaji wa aina gani kutokana na kuwa kinara kwa wachezaji waliofunga hat trick nyingi ndani ya muda mfupi katika Ligi Kuu Bara.
Kama umesahau, Aziz KI katika misimu mitatu amepiga hat trick tano, zikiwamo nne za Ligi Kuu Bara na moja ya Kombe la Shirikisho (FA) aliyofunga msimu huu wakati Yanga ikiizamisha na kutupa nje ya michuano Stand United kwa mabao 8-1.
Alianza kwa kufunga hat trick ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar walipoilaza mabao 5-0, kisha msimu uliopita kufunga mbili dhidi ya Azam wakati wanaifunga 3-2 na kuongeza nyingine walipoizamisha Tanzania Prisons kwa mabao 4-1 na msimu huu aliwatungua KMC iliyolala 4-1 hivi karibuni.

MABAO YA REKODI
Aziz KI alikuwa na mabao yenye umuhimu mkubwa ambapo la kwanza ambalo Yanga hawatalisahau ni lile alilowafunga Club African likiipa Yanga ushindi muhimu wa bao pekee ugenini Tunisia katika Kombe la Shirikisho Afrika na kuipeleka timu yake hatua ya makundi, msimu ambao ilienda hadi fainali.
Kiungo huyo pia alifunga bao lililozua utata katika mchezo dhidi Mamelodi Sundowns hatua ya robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambalo kama mwamuzi angekuwa makini lilikuwa linawapeleka Yanga hatua ya nusu fainali. Mechi hizo mbili za robo fainali ziliisha kwa matokeo ya 0-0 kabla ya Yanga kutolewa kwa penalti.
Ukiacha mabao hayo yatakayoendelea kukumbukwa na mashabiki wa Yanga, Aziz KI amekuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao yaliyoibeba timu katika Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na michuano hiyo ya CAF na alikuwa mmoja ya walioipeleka Yanga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25 tangu ilipotinga hatua hiyo mwaka 1998.
SIMBA MABAO MATATU
Taarifa ya Aziz KI kuondoka Yanga huenda zikawafurahisha watani wao, Simba ambao amewafunga mabao matatu akimfunga Aishi Manula mara mbili kwa frii-kiki timu yake ilitoka sare ya bao 1-1, kisha akamfunga katika ushindi wa mabao 5-1 mechi ya Novemba 5, 2003 na pia akamfunga kipa Ayoub Lakred kwenye ushindi wa mabao 2-1.
Mbali na Simba timu nyingine inayopumua kuondoka kwa Aziz Ki ni Azam kwani ni moja ya klabu aliyokuwa na bahati kuitungua tangu awepo nchini, ukiachana na ile hat-trick iliyowakata stimu Wanalambamba kwenye Uwanja wa nyumbani wa Azam Complex Oktoba 23, 2023.
Hii inaweza kuwa ni nyongeza tu ya alama ambazo Aziz Ki ameacha kwa mashabiki wa Yanga ni kile alichokifanya Februari mwaka huu kwa kuamua kumuoa mwanamitindo Mtanzania Hamisa Mobetto kwenye tukio la ndoa ambayo iliitingisha nchi kwa sherehe iliyoonyesha kuwa na matumizi makubwa ya fedha ikiwa mubashara nchi nzima.

KUIVAA MAN CITY, JUVE
Taarifa za Aziz Ki kuuzwa Wydad aliyoifuata usiku wa juzi, inampa nafasi ya kuliamsha katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inayoshirikisha timu 32 zilizopangwa katika makundi manane ya timu nne-nne.
Wydad imepangwa Kundi G sambamba na Manchester City ya England, Juventus ya Italia, Al Ain ya Falme za Kiarabu (UAE), michuano ikifanyikia Marekani na atajumuika na straika Mtanzania, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ aliyekuwa Fountain Gate.
Ratiba inaonyesha Wydad itaanza michuano hiyo Juni 18 dhidi ya Man City, Juni 22 itacheza na Juvenus kabla ya Juni 26 kumalizana na Al Ain na itakuwa ni nafasi kwa Aziz KI kuonyesha makeke.
Mabosi wa Yanga wamekuwa wasiri juu ya dili hilo, lakini ukweli ni kwamba Aziz Ki ameuzwa rasmi Wydad kwa dau linalotajwa kuwa ni nono, bila kuainishwa.

MSIKIE KOCHA MILOUD
Akizungumzia kuondoka kwa Aziz KI, kocha wa Yanga, Hamdi Miloud alisema kuwa na mchezaji mwenye kipaji kama kiungo huyo ni bahati kwa timu yao na hata kwa Ligi Kuu Bara na kwamba alama zake zitabaki kwa muda mrefu.
Miloud alisema Aziz KI kuondoka Yanga sio taarifa njema, lakini kwa kuwa ni hatua ya maendeleo lazima ipokewe huku akimtakia kila la kheri.
“Sikiliza, Aziz KI ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, kwa Ligi ya Tanzania au hata Yanga kuwa na mchezaji mwenye kipaji kikubwa kama huyu ni hatua kubwa, naweza kusema ni sawa na bahati,” alisema Miloud.
“Nimefanya naye kazi kwa muda mfupi, lakini huyu ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, mshindani anayeipenda kazi yake, ni taarifa mbaya inayoumiza kusikia mchezaji wa kipaji cha aina yake anaondoka sehemu unayoifanyia kazi, lakini kwa kuwa ni hatua ya kimaendeleo mnatakiwa kukubaliana nayo na kumtakia kila la kheri.”