
Dar es Salaam. Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema licha ya kudondosha pointi nyingi duru la kwanza bado ana nafasi ya kuipambania timu hiyo kutwaa taji msimu huu, huku akiweka wazi kuwa ana pointi sita kwa Simba na Yanga.
Azam ipo nafasi ya tatu katika msimamo baada ya kukusanya pointi 36 ikiwa mbele mchezo mmoja dhidi ya wapinzani wake Simba (40) na Yanga (39) ambazo pia zimemuacha pointi licha ya kuwa nyuma kwa mchezo mmoja.
Akizungumza na Mwananchi, Taoussi alisema duru la pili ni lala salama kwa kila timu inahitaji kukusanya pointi tatu muhimu kwenye kila mchezo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri mwisho wa msimu na wao kama Azam wanapambana kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kutwaa ubingwa msimu huu.
“Kudondosha pointi mzunguko wa kwanza haina maana tumeshakata tamaa bado tuna nafasi na ukizingatia washindani wetu Simba, Yanga tuna mechi nao mzunguko huu wa pili hatuwezi kufanya makosa kudondosha tena dhidi yao hadi kwa Simba ambayo ilifanikiwa kutufunga mzunguko wa kwanza,” alisema Taoussi na kuongeza;
“Ukitaka kushinda taji usikubali kuwa mnyonge mbele ya mshindani wako pointi nne ambazo wapo mbele yetu vinara wa ligi tatu tutazichukua kwao na kwa upande wa mabingwa watetezi pia ambao wanapambania kutetea taji lao tutahakikisha tunaendelea tulipoishia.”
Alisema duru la pili hawahitaji kufanya makosa kwa sababu kosa moja litawafanya washindwe kufikia malengo anapambana kuhakikisha anafanyia kazi mapungufu waliyoyaonyesha mzunguko wa kwanza kabla ya kurejea ngwe ya pili.
Azam mchezo wake wa kwanza inaanzia nyumbani dhidi ya KMC kitu ambacho kimemuibua Taoussi ambaye ameweka wazi kuwa ni ratiba nzuri kwake kuanzia nyumbani ili kutumia vyema uwanja wake kabla ya kumkabili mpinzani ugenini.
“Kuna faida kurejea uwanjani kwa kuanza na uwanja wa nyumbani ambao tumeufanyioa kazi kwa zaidi ya wiki mbili hili kwetu ni jambo zurio na mpinzani wetu tutaingia kwa kumuheshimu kwani pia anahitaji matokeo mazuri ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kucheza tena msimu ujao.”