
Dar es Salaam. Miaka 20 imepita tangu klabu ya Azam ilipoanzishwa Julai 23, 2004 ambapo mpaka sasa imeshiriki mashindano mengi tafauti ikiwemo Ligi Kuu Bara, CRDB Cup zamani kama FA Cup, Kagame Cup, Mapinduzi Cup, Ngao ya Jamii pamoja na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Ukiziacha Simba na Yanga ambazo ndizo klabu zenye mafanikio makubwa hapa Tanzania, Azam ni klabu ya tatu kwa ukubwa ikiwa imefanikiwa kushinda mataji mbalimbali ya mashindano tofauti ambayo imeshiriki tangu kuanzishwa kwake.
Mwaka 2014, hautasahaulika kwa wanalambalamba baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya wababe wa soka la Tanzania Simba na Yanga.
Azam walikuwa Mabigwa wa Ligi Kuu baada ya kukusanya jumla ya pointi 62 huku ikiwaacha nyuma Yanga waliokuwa na pointi 59, nafasi ya tatu ilishikwa na Mbeya City waliokuwa na pointi 49, wakati Simba walimaliza nafasi ya nne wakiwa na pointi 38.
Mashindano ya Mapinduzi Cup yanaweza yakawa ya kihistoria kwa matajiri wa Chamazi kwani ndiyo klabu inayoongoza kwa mataji ikiwa nayo matano ambayo waliyachukua mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.
Kwenye Mashindano ya Kagame Cup, Azam imeshinda mataji mawili kati ya mara nne walizoshiriki ambapo walitwaa mataji hayo mwaka 2015 wakiifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0, huku mwaka 2018 walinyanyua taji la pili kwa kuifunga Simba mabao 2-1.
Kwenye Kombe la CRDB Cup zamani kama ‘FA Cup’, Azam wameshinda taji moja pekee mwaka 2019 huku wakiwa wamecheza fainali nne.
Kwenye mashindano ya Ngao ya Jamii, Azam wamecheza fainali sita huku wakiwa mabingwa mara moja wakifanya hivyo mwaka 2016 walipoifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katika miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, Klabu ya Azam imefanikiwa kuweka rekodi mbalimbali ikiwemo ile ya kumaliza Ligi Kuu Bara mwaka 2014 walipokuwa Mabingwa bila kupoteza mchezo wowote sawa na Simba ambao pia waliwahi kufanya hivyo mwaka 2010.
Azam pia wanashikilia rekodi ya kuwa na mataji mengi ya Mapinduzi Cup ikiwa inaongoza kwa kubeba mataji matano mbele ya Simba yenye mataji matatu huku Yanga, Mtibwa Sugar na Mlandege wakiwa nayo mawili.
Msimu uliopita wa 2023/2024, Azam iliweka rekodi ya kumaliza Ligi Kuu kwa kukusanya pointi nyingi zaidi tofauti na misimu mingine ambapo walikusanya jumla ya pointi 69 lakini pia iliweka rekodi ya kupachika idadi kubwa ya mabao katika msimu mmoja wa Ligi ambapo ilipachika mabao 63.
Klabu ya Azam imekuwa ikikutana na kikwazo kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ambako wamekuwa wakiondolewa katika hatua za mwanzoni jambo linalosababisha wanalambalamba hao kukosa kuingia hatua ya makundi tangu walipoanza maisha ya soka mwaka 2004.
Mpaka sasa Klabu ya Azam imeshanolewa na makocha 30 ambao walihudumu vipindi tofauti kwenye viunga vya Chamazi huku makocha sita wakiwa ni Watanzania wakati 24 wakitokea mataifa mengine ya Afrika na nje ya Afrika.
Kwa sasa Azam ipo chini ya kocha Rachid Taoussi raia wa Morocco ambaye alichukua nafasi ya Youssouph Dabo aliyefungashiwa virago Septemba 3, 2024 akiwa ameitumikia Azam kwa siku 422.