
KAMA mambo yataenda kama yalivyo, Azam FC ina mpango wa kumtema kipa Mohamed Mustafa raia wa Sudan sababu ikitajwa ni kufanya makosa mengi akiwa golini, hivyo umeanza mchakato wa kumsaka mbadala wake atakayewasaidia msimu ujao.
Chanzo cha ndani kutoka Azam kinasema tayari uongozi wa timu hiyo umeanza mazungumzo na kipa namba moja wa As Vita ya DR Congo, Farid Ouedraogo na kama dili likitiki basi Mustafa atapewa mkono wa baibai.
Azam ilimsajili Mustafa kutoka Al-Hilal ya nchini kwao Sudan kwa msimu huu amecheza mechi 17, dakika 1530 karuhusu mabao 10 ana clean sheet 10, lakini bado uongozi wa timu hiyo umeona kuna haja ya kusaka kipa mwingine.
“Kiwango chake wakati anajiunga na Azam kilikuwa kikubwa tofauti na msimu huu ambapo kuna makosa mengi anayafanya, haimanishi kwamba kaishiwa kiwango ila inatokea wakati mwingine mchezaji kuchoka, ndio maana kumewekwa usajili mkubwa na wa dirisha dogo ili timu ziboreshe vikosi vyao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Tumekuwa tukikifuatilia kiwango cha kipa wa As Vita Ouedraogo anadaka kwa ubora wa hali ya juu, mzuri wa kuona mipira ya mbali, anajua kuanzisha mashambulizi, kiongozi dhidi ya wachezaji wengine na hafungiki kirahisi,”kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Azam na kusisitiza kwamba bado jambo hilo linafanywa kwa usiri mkubwa.
Chanzo hicho kilisema nje na kipa watafanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chao cha kuwaacha baadhi ya wachezaji na kuwasajili wengine wapya ambao wataisaidia timu hiyo kufikia malengo yao.