
Dar es Salaam. Matumaini ya Asasi za Kiraia kuhusu hatima ya vita vinavyoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC), yapo mikononi mwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hilo linatokana na kile kilichoelezwa na Jumuiya ya Asasi za Kiraia Ukanda wa Maziwa Makuu kuwa, SADC na EAC zina nafasi na ushawishi mkubwa katika kumaliza kile kinachoendelea DRC na hali ya kushutumiana baina ya taifa hilo na Rwanda.
Mtazamo wa asasi hizo, unakuja ikiwa ni siku moja kabla ya wakuu wa nchi za EAC na SADC kukutana Dar es Salaam, kujadili kuhusu namna ya kumaliza mgogoro huo.
Katika mkutano huo wa ngazi ya juu, Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, wa Rwanda Paul Kagame, wa Kenya, William Ruto, wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na wengine watakaa meza moja kuzungumza hatima ya mgogoro huo.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ndiye mwenyeji, jambo linaloongeza matumaini ya kumalizwa kwa mgogoro unaoendelea, kutokana na historia ya Tanzania katika kuongoza na hatimaye kupata suluhu ya migogoro ya mataifa mbalimbali kwa mazungumzo.
Mbali na kuonyesha matumaini hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Asasi za Kiraia Ukanda wa Maziwa Makuu, Joseph Butiku amesema nao wamejifungia kujadili kuhusu mgogoro huo na watawasilisha maazimio yao kwa wakuu wa nchi kesho.
Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Februari 7, 2025 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Asasi za Kiraia za Ukanda wa Maziwa Makuu, Butiku katika kikao cha dharura walichoketi kujadili suluhu ya migogoro unaoendelea Mashariki kwa DRC dhidi ya Kundi la M23.
Kwa mujibu wa Butiku, wamekutana kama muungano wa asasi za kiraia katika nchi za maziwa makuu, kutilia mkazo hicho kitakachoazimiwa na wakuu wa nchi.
Amesema wana matumaini kuwa mazungumzo yatajielekeza katika kurejesha amani, kwa sababu si nia ya kiongozi yeyote kutoka nchi wanachama wa SADC wala EAC kuona vita inaendelea.
Lakini, kabla ya maazimio ya wakuu wa nchi za EAC na SADC kesho, amesema wanajadili na watawasilisha mapendelezo yao kwa viongozi hao ili kuwa na sauti moja.
“Nilipigiwa simu na viongozi wa asasi hizi, kwa umoja wetu tukakubaliana tukutane kwanza kuunga mkono juhudi za wakuu wa nchi katika kutafuta suluhu ya mgogoro huu,” ameeleza.
Amesema kwa kuwa uamuzi utakaotolewa na wakuu wa nchi utakuwa wa viongozi wakuu wanaamini utalenga kumaliza vita.
“Sijawa na uhakika kama utaratibu utatuwezesha kuingia ndani ya mkutano, lakini hata tusipokwenda tunaruhusiwa kupeleka taarifa yetu,” amesema Butiku.
Akieleza sababu ya imani yake kwa SADC na EAC kuwa zitamaliza mgogoro huo, amesema kwa sababu zina kanuni na muundo mzuri wa kusimamia amani kwa nchi zake wanachama.
Kiongozi wa Umoja wa Asasi za Kiraia nchini Kenya, Kennedy Walusala amesema kwa sababu DRC ni nchi mwanachama wa EAC na Taifa la Afrika, hawana budi kushinikiza amani ya watu wake.
Amesema watu wamepata shida nchini DRC hasa Mji wa Goma, hivyo wameona asasi kutoka ukanda wa maziwa makuu waungane na wakuu wa nchi kutafuta amani.
Amesema baada ya kikao cha wakuu wa nchi Jumapili Februari 9, 2025 wanatarajia kukutana kwa tathmini ya hatua iliyofikiwa.
Hali ilivyo DRC
Akisimulia hali ilivyo nchini DRC, raia wa nchi hiyo, Eloi Bugoye amesema vita vilianzia Bunagana katika mpaka wa DRC, Uganda na Rwanda na iliendelea hadi kukaribia Goma na baadaye Goma kushikiliwa.
Amesema kwa sasa Mji wa Kivu nao umeanza kuwa kwenye shida na maeneo yake ya jirani.
Eneo salama zaidi ni Mji Mkuu wa nchi hiyo Kinshasa na ndiko viongozi hukaa kujadili mambo mbalimbali ya kusaka amani.
“Hali ya vita inaleta shida kwa sababu wakimbizi wanaongezeka, mauaji yanaongezeka, wapo wanaokufa kwa mabomu wengine kwa njaa. Hata biashara zimesimama kwa sababu wanamgambo wa M23 wamepora,” amesema.
Amesema wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa wameshaondoka mjini Goma kukimbilia nchi za jirani.
Kwa hali ilivyo, amesema wanajua vita ilianza lini lakini hawajui lini itakwisha huku akisisitiza iwapo hali itaachwa kama ilivyo mambo yatakuwa mabaya zaidi baadaye.
Amesisitiza hafikirii kuwa, kuuawa kwa raia kunamfaidisha yeyote katika vita hiyo, hivyo ni muhimu amani ipatikane.
Bugoye ambaye pia ni mtaalamu wa sheria nchini DRC, amesema anatarajia itatokea sauti ya pamoja itakayowasilishwa kwa wakuu wa nchi.