AyatullahAli Sistani asikitishwa na kushindwa jamii ya kimataifa kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni

Marja’ wa ngazi ya juu ya Mashia wa Iraq imeeleza masikitiko yake kuhusu kushindwa jamii ya kimataifa na taasisi husika katika kuzuia hujuma za kikatili za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon.

Kuanzia tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni ukiungwa mkono kikamilifu na nchi za Magharibi, ulianzisha mauaji makubwa ya umati katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina ambapo kimya kikubwa cha jamii ya kimataifa, na taasisi za kutetea haki za binadamu katika kukabiliana na jinai za kinyama za  utawala huo ghasibu, kimepelekea kuendelezwa mauaji hayo dhidi ya wanawake na watoto wa Kipalestina.

Tangu kuanza mashambulizi hayo tarehe 7 Oktoba, Wapalestina 43,374 wameuawa shahidi na wengine 102,261 wamejeruhiwa.

Kadhalika, tangu tarehe 23 Septemba jeshi la Kizayuni limefanya mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon na kusababisha kuuawa shahidi zaidi ya watu elfu tatu.

Kwa mujibu wa kanali ya Sahab, Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marja Mkuu wa Mashia wa Iraq, ameeleza masikitiko yake makubwa katika mazungumzo yake na Mohammad al Hassaan, Mkuu mpya wa Ujumbe wa Misaada ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI), ambaye pia ni Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo, na ujumbe alioandamana nao, kuhusu maafa ya sasa nchini Lebanon na katika Ukanda wa Gaza, na kusikitishwa sana na kushindwa jamii ya kimataifa na taasisi husika katika kuzuia uchokozi wa kinyama unaofanywa na utawala huo pandikizi.

Ayatullah Sayyid Ali Sistani pia, amesema: ‘Wairaqi, hasa wasomi, wanapaswa kufanya kila wawezalo kushinda vikwazo na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia mustakabali bora kwa manufaa ya nchi yao.’