
Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Kiongozi wa juu wa kidini na Marjaa-Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq amelaani shambulio la magaidi wa kitakfiri dhidi ya kundi la watu wa mji wa Shia wa Parachinar, Pakistan.
Ayatullah Sistani ameitaka serikali ya Pakistan kuchukua hatua zinazohitajika ili kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa eneo hilo dhidi ya uhalifu wa makundi ya kigaidi na kuwadhaminia usalama wao.
Ofisi ya kiongozi huyo wa juu wa kidini na Marjaa-Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq imetoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika shambulio hilo la kigaidi na kuwatakia afya njema majeruhi.
Sehemu moja ya taarifa ya ofisi ya Ayatullah Sistani imesema: Ninaitaka serikali ya Pakistan kuchukua hatua zinazohitajika kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa dhidi ya dhulma na jinai za makundi ya kigaidi na kutoruhusu waumini wasio na hatia kuandamwa kwa mashambulizi ya kikatili na ya kinyama mara kwa mara na makundi yenye misimamo mikali.
Waislamu wa madhehebu ya Shia wapatao 42 waliuawa shahidi hivi karibuni katika shambulio la kigaidi walipokuwa wakisafiri kutoka katika mji wa kaskazini magharibi wa Parachinar kuelekea Khyber Pakhtunkhwa nchini Pakistan.