Ayatullah Khatami: Visiwa vitatu ni milki ya Iran, vilikuwa na vitaendelea kuwa hivyo

Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesisitiza kuwa, visiwa vitatu vya Bu Musa, Tomb Kubwa na Tomb Ndogo ni milki ya Iran, vilikuwa hivyo tangu zamani na vitaendelea daima kuwa hivyo katika siku za usoni.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesisitiza hayo na huku akigusia madai yaliyotolewa tena hivi karibuni kuhusu visiwa hivyo vitatu vya Iran amesema kuwa, kuanzia miaka ya 1971-1972 madai kuhusu visiwa hivyo vitatu vya Iran lilizuka baada ya mfalme Shah wa Iran kukubali kuipoteza Bahrain. Ingawa kuanzia wakati huo hadi hivi sasa, hakuna mwaka wowote unaopita bila ya kuzungumziwa visiwa hivyo vitatu vya Iran lakini hivi sasa hali ni tofauti kwani nchi tatu za Ulaya zimejiingiza kwenye suala hilo dhidi ya Iran.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema kuwa, sababu inayozifanya nchi za Ulaya kuchukua msimamo ulio dhidi ya Iran kuhusu visiwa hivyo vitatu ni kutaka kuufurahisha utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini hivi sasa Iran ina nguvu kubwa zaidi na kamwe haiko tayari kupoteza hata shibri moja ya ardhi yake. 

Visiwa vitatu vya Iran katika Ghuba ya Uajemi

Amma kuhusu mapambano dhidi ya dhulma, Ayatullah Ahmad Khatami amesema kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyaamrisha mataifa ya dunia kusimama imara kupambana na dhulma na ukandamizaji na kwamba Allah Yuko pamoja na wanaopambana katika njia Yake.

Amesema: Kwa kuzingatia hayo tunasema kwa yakini kwamba utawala katili na dhalimuwa Israel utaangamia kama walivyoangamia madhalimu wote na kwa hakika kambi ya Muqawama ndiye mshindi. 

Aidha amenukuu miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kwamba ushindi ni wa kambi ya haki dhidi ya batili na kusisitiza kuwa, ushahidi wa miongozo ya Kiongozi Muadhamu ni aya ya 56 ya Suratul Maaidah ambayo inasema: Basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kushinda.