Ayatullah Khatami: Uamuzi wa Bodi ya Magavana wa IAEA dhidi ya Iran umefuata matakwa ya Wazayuni

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amelichukulia azimio la Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran kuwa linafuata matakwa ya utawala haramu wa Israel.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami, Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema hayo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa katika mji mkuu Tehran na kueleza kwamba, ulimwengu unapaswa kujua; taarifa hiyo ni ya kuunga mkono utawala wa Kizayuni, na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ilitaka kusema kwamba inasonga mbele katika mstari wa utawala huo wa Kizayuni muuaji, na chombo cha kidiplomasia cha Iran kinatarajiwa kutoa jibu thabiti na la kishindo. kwa azimio hili.

Ayatullah Khatami ameashiria kuwa pamoja Marekani na Israel na himayay na uungaji mkono wake kwa mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya Gaza na kusema kwamba, wakati Marekani inapopiga kura ya turufu katika azimio la kusitisha mapigano huko Gaza, ni ishara ya ukatili wa Marekani.

Katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki jana Novemba 21, kwa shinikizo na ung’ang’anizi wa nchi tatu za Ulaya na Marekani, na licha ya kutoungwa mkono na karibu nusu ya nchi wanachama, limepitishwa azimio lisilo la kauli moja kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.