Aweso awataka Dawasa wasizoee matatizo ya wananchi

Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kutokubali kuzoea matatizo ya wananchi bali wayashughulikie kwa kasi kubwa.

Ameyasema hayo leo Jumanne, Februari 18, 2025 katika kikao kazi kati ya Dawasa na wenyeviti wa serikali za mitaa wilaya ya Kinondoni akisema kutoa taarifa kutasaidia kuwa na uelewa wa changamoto iliyopo na inavyofanyiwa kazi.

“Niwasii sana haya mashirikiano yakiboreshwa zaidi yatachangia kwa kiasi kikubwa kutoa ulinzi wa huduma ya maji, kwani viongozi hao watailinda huduma hiyo kwa wivu mkubwa,” amesema Aweso.

Waziri huyo amesema mawasiliano kati ya Dawasa na wenyeviti hao wa serikali za mitaa yanatakiwa kuboreshwa ili taarifa rasmi za kukatika ama kuharibika kwa pampu za maji ziwe zinawafikia kwa wakati jambo litakaloondoa taharuki kwa wananchi kwani wenyeviti watawapa taarifa watumiaji wa huduma ya maji.

Pia, amewapongeza Dawasa kwa kusimamia ipasavyo mradi wa maji kidunda akieleza kuwa mradi huo utasaidia zaidi kuongezeka kwa upatikanaji wa maji katika maeneo mengi hasa ya Kinyerezi, Tabata na maeneo mengi zaidi.

“Dawasa msizoee matatizo ya wananchi, hakikisheni kuwa huduma ya maji inapatikana kwa urahisi, jisikieni raha kuona kila maeneo maji safi na salama yawe yanapatikana kila wakati, hiki ndio kipimo cha utendaji kazi wa wenu,” amesema Aweso.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema maji ni uhai, hivyo yakikosekana maisha yanaweza kuwa hatarini, maji hayana mbadala, ni kitu cha muhimu kuhakikisha kuwa yanapatikana na yanakuwa ya kutosha.

Amesema usambazaji wa maji katika wilaya ya Kinondoni kwa sasa ni wa asilimia 97 na hii ni kwa sababu usiku na mchana watendaji wa Dawasa wamekuwa wakihakikisha kuwa wanafuatilia na kusambaza maji katika kila kata na vitongoji.

“Niwajibu wetu sisi wananchi wa Kinondoni kuilinda dawasa kwa wivu mkubwa, kwani huduma wanayotupatia ni muhimu sana kwetu, maji yakikosekana kila jambo linaweza kusimama, hivyo mashirikiano haya yataimarisha huduma ya maji Kinondoni,” amesema.

Amesema si jambo zuri kwa watu wasiokuwa na mapenzi mema kufanya wizi wa maji, wengine wakiiba mita na hata kukata mabomba, hivyo mashirikiano kati ya wenyeviti na Dawasa yataimarisha ulinzi dhidi ya wale wasiokuwa na mapenzi mema.

Awali, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amesema kuboreka kwa ushirikiano kati ya Mamlaka na wenyeviti wa serikali za mitaa kutatatua changamoto mbalimbali kwani zingine zisizofikiwa na Dawasa zitatolewa taarifa kupitia viongozi hao.

Amesema wenyeviti wa serikali za mitaa ndio wanaoishi na wananchi ambao ni watumiaji wa huduza ya maji safi na salama akieleza kuwa kwa sasa Wilaya ya Kinondoni ina wastani kaya laki tatu huku usambazaji wa maji ukiwafikia wananchi kwa Asilimia 97.

“Tunapozungumza kuhusu maboresho ya huduma ya maji hatutaki kubahatisha, hivyo tunaamini wenyeviti hawa watatusaidia kuwa mabalozi na walinzi wa maji huko mitaani,” amesema Bwire.