Aweso asimulia magumu mradi wa maji uliokwama miaka 19

Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameeleza magumu aliyopitia na watendaji wengine wa Serikali katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe hadi kusababisha wengine wafukuzwe kazi.

Amesema ni katika utekelezaji wa mradi huo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliahidi kuacha kazi iwapo kazi hazitakwenda sawa, jambo lililomfanya Aweso ahisi kutenguliwa katika wadhifa wake.

Dk Mpango alitoa ahadi ya kuacha kazi, Machi 21 mwaka jana, akieleza hayuko tayari kurudi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kumweleza maji hayatoki.

“Kila mtu atimize wajibu wake, kurudi kwa Rais kwamba maji hayatoki… mimi nitaacha kazi, hao wengine sijui, Katibu Mkuu na waziri wake mimi sijui, kwa hiyo tuelewane vizuri,” alisema Dk Mpango.

Hata hivyo, yote hayo yametokana na kusuasua kwa mradi huo, ulioanza tangu mwaka 2014, lakini hatimaye awamu ya kwanza inakamilika mwaka huu.

Aweso ametaja magumu hayo, leo Jumapili, Machi 9, 2025 alipotoa salamu za Wizara ya Maji wakati wa hafla ya kuzindua mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe.

Gumu la kwanza kwa mujibu wa Aweso, ni pale unapoteuliwa katika Wizara ya Maji, jambo la kwanza utakaloambiwa ni mradi huo, vivyo hivyo la pili na tatu.

“Nakumbuka siku moja tulikuwa kwenye kipindi cha kurasa nilikuwa nazungumza mafanikio ya sekta, mradi huu niliukwepa kidogo, ulipiga simu (Rais Samia Suluhu Hassan) mubashara ukasema waziri wangu umeongea vizuri lakini Same-Mwanga-Korogwe sijakusikia naomba uende ukatekeleze wananchi wakapate maji,” amesema.

Amesema hayo yote maana yake Rais Samia ana mapenzi ya dhati na wananchi wa maeneo yanayoguswa na mradi huo.

Katika maelezo yake, amekumbushia magumu mengine akisema mradi huo uliwatesa hata viongozi wakuu akiwemo Dk Mpango aliyeahidi kujiuzulu.

“Alikuja hakuwa na maneo mengine alitwambia, wana-Mwanga, wana-Same na Korogwe wanachohitaji maji na mkishindwa kuleta maji hadi Juni mimi nitajiuzulu, nikasema sasa nishaliwa kichwa.

“Kila mkeka ukitoka tunachungulia, lakini kwa dhati ya moyo hakuna jambo nililojifunza kama uvumilivu, umetuvumilia hadi kazi tumeimaliza,” amesema.

Katika kusisitiza magumu hayo, Aweso amesema kazi haikuwa rahisi kwa sababu wapo watendaji waliofukuzwa kazi na wengine wamelazwa polisi na ametumia jukwaa hilo kuwaomba radhi wote waliokwazana nao kwa shughuli hiyo.

“Ilikuwa kwa nia njema kuhakikisha maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu yanatekelezwa,” amesema.

Amesema waliwahi kwenda kwa Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya kutaka historia ya mradi na aliwaeleza kwa kina.

Sambamba na hilo, amesema ulifika wakati hadi alikuwa akipishana na wabunge wa maeneo yatakayonufaika kwa ajili ya mradi huo lakini sasa umekamilika.

“Tumezungumza na viongozi wa kimila, mheshimiwa Rais hapa hadi matambiko yamefanyika kuhakikisha mradi unakamilika,” amesema huku vicheko vikiwata wahudhuriaji wa shughuli hiyo.

Ametumia jukwaa hilo kuwataka watendaji wa mamlaka za maji katika maeneo yanayonufaika, waache kuwakatia maji wakazi wote.

Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumapili, Machi 9, 2025 amezindua mradi wa maji wa Same -Mwanga – Korogwe katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Uzinduzi huo uliofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro, pia umeshuhudiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema mradi huo unatarajiwa kuvihudumia vijiji 38 kati ya hivyo, 17 vipo wilayani Mwanga, 16 Same, Kilimanjaro na vitano wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Katika vijiji hivyo, amesema wananchi 456,931 watafikiwa na huduma hiyo ya maji kulingana na usanifu wake na kwamba lita milioni 103.65 zitazalishwa.

Mgawanyiko wa lita hizo, amesema milioni 60.2 kwa ajili ya Same, milioni 40.2 kwa ajili ya Mwanga na milioni 3.3 kwa ajili ya vijiji vya Korogwe.

Katika kuutekeleza mradi huo, amesema Serikali ilipata mkopo kutoka taasisi mbalimbali ikiwamo Kuwait Fund na Saudi Fund.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo ulianza mwaka 2014 na umekamilika ukihusisha ujenzi wa chanzo, bomba la kusafirisha maji ghafi na tenki la lita milioni mbili.

Mwajuma amesema kipande cha pili cha awamu hiyo kimehusisha kituo cha kusukuma maji, bomba kuu la kusafirisha maji na matenki ya kuhifadhi maji na yote yametekelezwa.

Ameeleza tangu kuanza kwa awamu ya kwanza, mwaka 2014 tayari Sh406.1 bilioni zimetumika kwa ajili ya kulipa makandarasi na washauri.

“Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo cha kuzalisha lita milioni 103, mtambo wa kusafisha maji lita milioni 51.65, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji kilomita 81.8 na kulaza bomba la kusambaza maji megawati 16 na matanki saba ya kuhifadhi maji kuanzia lita 300,000 hadi milioni tisa,” amesema.

Katika taarifa yake hiyo, amesema vijiji tisa vya Njiapanda, Kisangara, Lembeni, Mbambua, Kiruru, Kiverenge, Mgagao, Njoro na Ishinde vimeanza kupata maji.

Amesema taratibu za kuhakikisha wananchi wa vijiji vilivyobaki wanapata maji zinaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *