Aucho, Camara hali tete Yanga, Simba

NYOTA wawili muhimu katika vikosi vya Yanga na Simba, kiungo Khalid Aucho na kipa Moussa Camara wameibua hofu katika timu hizo kutokana na pancha zao.

Mbali na nyota hao, pia kuna beki wa kati Che Malone Fondoh ambaye ni rasmi ataikosa Simba katika michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry.

Simba ambayo Alhamisi hii itacheza na Bigman katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya hapo inatarajiwa kuanza safari ya kwenda Misri kuifuata Al Masry, mechi yao ikipangwa kufanyika Aprili 2.

Kuelekea mchezo huo, kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara, kuna juhudi kubwa zinafanyika ili awepo langoni kufuatia majeraha ya misuli aliyoyapata katika mchezo wa Mzizima Dabi dhidi ya Azam, Februari 24 baada ya kushindwa kusimama langoni kwenye timu yake ya taifa ya Guinea ambapo licha ya kuitwa aliishia jukwaani.

Simba haikutaka kumruhusu Camara kwenda kujiunga na timu ya Taifa ikihofia wanaweza kulazimisha kucheza na akachelewa kupona zaidi lakini kutokana na kanuni za Fifa zikawabana, Wekundu hao walilazimika kumuachia akajiunge tu hivyohivyo.

Hata hivyo, benchi la ufundi la Guinea halikuweza kufanya lolote kumnusuru kipa huyo chaguo la kwanza kusimama langoni kwani aliishia kufanya mazoezi mepesi huku pia akipatiwa matibabu majeraha yake ya mkono.

Camara amewafunika makipa wenzake aliowakuta kama Aishi Manula, Ally Salum, Hussein Abel, akipata nafasi ya kuanza mara kwa mara chini ya kocha Fadlu Davids.

Na anaongoza kwa kuwa na ‘clean sheet’ 15 mpaka sasa, akiwa ndiye kipa bora, akimzidi Djigui Diarra mwenye nazo 11, akiwa amecheza mechi 21 kati ya 22 ilizocheza Simba, akiifikia rekodi ya Ley Matampi kipa bora wa msimu uliopita kutoka Coastal Union.

Hatua makundi Kombe la Shirikisho, Camara alicheza mechi zote sita sawa na dakika 540, huku katika timu ya Taifa ya Guinea mechi zilizopita akicheza dakika zote pia.

Camara amethibitisha kwamba kukosa kwake mechi hizo kunatokana na kwamba bado hajawa sawa; “Bado sijawa sawasawa lakini maendeleo sio mabaya namshukuru Mungu, nafanya mazoezi kidogo sana lakini nikiwa huku napata matibabu kama kawaida,” alisema.

“Sitacheza hizi mechi mbili kutokana na hali yangu na mechi hizi zikimalizika nitarudi Tanzania kuendelea na ratiba za matibabu na mengineyo.

“Siwezi kusema kwamba mechi nyingine hasa hizo za robo fainali nitazikosa lakini mashabiki watulie hali yangu sio mbaya sana kila kitu kitakwenda sawa.”

 KUHUSU AUCHO

Khalid Aucho naye ameshtua kutokana na kupata jeraha la misuli akiwa timu ya Taifa. Aliukosa mchezo ambao Uganda ilishinda bao 1-0 dhidi ya Guinea kutokana na jeraha hilo la misuli.

Jeraha la kiungo huyo tegemeo Jangwani, limempasua kichwa kocha wa Yanga, Hamdi Miloud, ambaye amesema licha ya timu yake kuwa na mastaa wengi bora ila Mganda huyo bado ni wa muhimu hasa kwenye mechi zilizosalia.

Kwenye ligi Aucho ana rekodi ya kucheza mechi 19 kati ya 22 ambazo kikosi cha Yanga kimecheza hadi sasa, huku akifikisha dakika 1502, akiwa amefunga bao moja.

“Bado mashindano ya kuwania ubingwa wa ligi yanaendelea, hivyo mimi kama kocha natamani mastaa wangu wote wawe timamu ili niweze kuwa na kikosi kipana zaidi.

“Naelewa kuwa Yanga ina mastaa wengi, ila kumkosa kiungo kama Aucho ni wakati mgumu, kwani pengo lake sio rahisi kuzibika, licha ya wachezaji wenzake kuwa na bora pia.”

Katika eneo analochezea Aucho yuko na Mudathir Yahya, Duke Abuya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Jonas Mkude, huku akiwa ndiye kiungo mwenye rekodi kubwa ya kucheza muda mrefu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *