Auawa kwa kuchomwa visu na ‘house boy’ kwa madai ya kutompa penzi

Moshi. Mwanafunzi wa Chuo cha Utalii Marangu, mkoani Kilimanjaro, Clara Kimathi (21)  amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na ‘house boy’ wa familia aliyokuwa akiishi kwa madai ya kukataa kumpa penzi.

Mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na moja ya familia iliyopo kitongoji cha Mieresini, Kata ya Makuyuni Wilaya ya Moshi baada ya baba na mama yake kufariki dunia miaka michache iliyopita.

Inaelezwa kuwa baada ya mwanafunzi huyo kujeruhiwa Desemba 5 mwaka jana, alikuwa amelazwa Hospitali ya KCMC kwa zaidi ya miezi miwili ambapo hali yake haikutengamaa kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata, ambapo inadaiwa alichomwa visu vitano vya tumboni, mgongoni na kusababisha utumbo kutoka nje na ilipofika Februari 25, mwaka huu alifariki dunia.

Akizungumza na Mwananchi digital leo Machi Mosi, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Desemba 5, mwaka jana na tayari hatua kadhaa za kisheria zilishachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.

“Desemba 5, 2024 saa tano na nusu huko maeneo ya Mieresini Kata ya Makuyuni, Himo binti aitwaye Clara Kimati (21) mwanachuo cha utalii Marangu alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali upande wa kushoto na tumboni na kijana wa kazi za ndani,”amesema Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amesema kuwa, chanzo cha tukio hilo ni baada ya marehemu kumkatalia penzi ‘house boy’huyo.

“Kiini cha tukio hili ni kumtaka kimapenzi marehemu kwa nguvu, mbinu iliyotumika ni kumjeruhi marehemu  kwa kumkata na kitu chenye nchi kali upande wa kushoto na tumboni na mtuhumiwa aitwaye Ezekiel Komba  baada ya kutenda kosa hilo na alitaka kujiua kwa kujikata koromeo,” amesema Kamanda.

Kamanda Maigwa amesema taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo wamezipata Februari 28, mwaka huu.

Baba mlezi wa Clara asimulia tukio lilivyotokea

Severene Oisso, ambaye ni baba mlezi wa Clara (marehemu) anayeishi kitongoji cha Mieresini, Himo amesema binti huyo wamekuwa wakiishi naye tangu mwaka 2019, mama yake alipofariki dunia na alikuwa afanye mitihani yake ya kumaliza chuo Desemba mwaka jana.

Anasema kuwa, Desemba 5, mwaka jana yeye na mkewe hawakuwepo nyumbani na mfanyakazi wao wa  ndani ‘house boy’ ndiye aliyebaki wakati Clara (marehemu) hayupo.

Ameeleza kuwa, wakati Clara anarudi chuo saa tisa alasiri walikuwa wao peke yao nyumbani, hivyo ‘house boy’ akatumia fursa hiyo kumtaka kwa nguvu kimapenzi.

“Huyu kijana alikuwa amekaa kwangu  miezi mwili, bahati mbaya sisi siku ya tukio tukiwa kwenye pilikapilika za kutafuta riziki, nilimwacha Clara akiwa anaenda chuoni  na huyu kijana anaendelea na shughuli zake za hapa nyumbani.

“Sasa ilipofika jioni wakati narudi nyumbani niligonga geti halikufunguliwa, kumbe huyu binti alivyokwenda chumbani baada ya kurudi chuo yule kijana alifunga geti zote na kwenda kumtaka kwa nguvu kimapenzi chumbani kwake, katika zile purukushani ndio kukatokea hayo yaliyotokea,” amesema.

Anasema kutokana na geti kubwa kutofunguliwa, ilimlazimu azunguke nyuma ya nyumba apitie geti dogo.

“Chumbani kwa Clara niliona taa zinawaka saa kumi kasoro hivi, wakati huo Clara analia huku akisema anakufa, nilifungua mlango na kukuta binti amelala kwenye damu yake, akaniambia baba nakufa Ezekiel amenikata baba, kanipigia na kunikatakata nakufa,” amesimulia baba huyo.

Aidha, amesema alimuwahisha Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, baadaye akahamishiwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi na kisha hospitali ya KCMC ambako alifariki dunia.

Akizungumza baba mdogo wa marehemu, Onesmo Kimathi amesema baada ya kupata taarifa za mwanaye huyo, alifika Hospitali ya KCMC na kumkuta akiwa kwenye hali mbaya hawezi kutembea wala kukaa kutokana na kujeruhiwa uti wa mgongo, huku tumbo likiwa limechomwa visu vitano na utumbo umetoka nje.

“Nilipofika hospitali ya KCMC, marehemu alikuwa amejeruhiwa vibaya sehemu za mkono, mgongoni na visu vitano tumboni na utumbo ulitoka nje, hali yake ilikuwa ni mbaya hata kuzungumza alikuwa hawezi,”amesema mzee Kimathi

Amesema, kabla ya kukutwa na madhila hayo alimwambia mwaka huu anamaliza chuo na atarudi nyumbani kwenda kukaa na wadogo zake.

Mwili wa mwanafunzi huyo unatarajiwa kuzikwa wiki ijayo kwenye sehemu ya makaburi ya wazazi wake.