Auawa akigombea mke wa mtu

Kenya. Katika tukio la kushangaza Kevin Ouma ameuawa kwa kile kilichotajwa kugombea mke wa mtu. 

Ouma mwenye umri wa miaka 37 ameuawa wakati akikatana mapanga na mwanaume mwingine ambaye alikutana naye kwenye ahadi ya kukutana na mwanamke huyo.
Tukio hilo limetokea eneo la North East Kadem, Kaunti Ndogo ya Nyatike Kenya Jumatatu ya Machi 31, 2025.

Kwa lugha rahisi mwanamke huyo ambaye jina lake halijafahamika ‘amegonganisha magari’ ambayo ni michepuko wake. 

Ilivyokuwa

Tovuti ya Citizen Digital ya nchini humo ikimnukuu Mkuu wa eneo, Voshastar Akal akisema marehemu Ouma na mshukiwa wa mauaji, Johnson Ochieng ambaye pia alipata majeraha mabaya ya panga walikuwa wakigombania mwanamke aliyeolewa.

Akal amesema walikutana nyumbani kwa mwanamke huyo, ambapo wote wawili waliripotiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye kwa siri.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu Ouma alikuwa amepanga kukutana na mwanamke huyo usiku huo nyumbani kwake. 

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuwasili, mshukiwa Ochieng alifika pia kumuona mwanamke huyo, jambo lililosababisha kuzuka kwa ugomvi mkali.

Kwa kutumia silaha butu, wawili hao walipigana vikali, na hatimaye Ouma alipigwa na silaha hiyo kifuani na kufariki papo hapo. 

Mshukiwa pia alipata majeraha mabaya na kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Migori Level Four.

Familia yachoma nyumba

Mkuu wa eneo, Akal, ameongeza kwamba kutokana na hasira familia ya marehemu iliamua kuvamia na kuchoma nyumba ya mwanamke huyo, ambaye mumewe anaripotiwa kuwa mfanyakazi nje ya Kaunti ya Migori.

Kwa sasa polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo lililowaacha watu vinywa wazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *