Mkuu wa Umoja wa Afrika amelitaka Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua madhubuti za kukabilian na marufuku iliyowekwa na Israel dhidi ya shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina, UNRWA.
Katika taarifa yake, Moussa Faki Mahamat amesema kuwa, iwapo marufuku hiyo ya Israel itatekelezwa itakwamisha misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwa watu wa Palestina ambao tayari hivi sasa wanateseka mno kutokana na jinai za Israel.
Amesisitiza kuwa, Israel inapaswa kuheshimu majukumu yake ya kimataifa ambayo yanaamuru kuruhusiwa shirika la UNRWA ambacho ni chombo kilichoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1949 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Palestina kufanya kazi zake kwa uhuru kamili.

Mwenyekiti huyo wa AU ameashiria pia sheria ya kimataifa ya kibinadamu ambayo inaamuru kupelekewa misaada raia wwenye mahitaji, akiitaka Israel kuheshimu sheria za kimataifa.
Jeshi la Israel linaendelea kufanya jinai na mashambulizi makubwa katika Ukanda wa Ghaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023 licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitaka kukomesha mara moja jinai zake hizo.
Israel inadai kuwa wafanyakazi wa UNRWA walihusika katika operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoendeshwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS tarehe 7 Oktoba 2023 na kutoa pigo kubwa mno la kijeshi, kiusalama, kisiasa, kiuchumi na kiitibari kwa utawala wa Kizayuni; pigo ambalo haliwezi kabisa kusahaulika katika historia.
Madai hayo ya Israel yamekanushwa vikali kama ambavyo utawala wa Kizayuni unaendelea kulaaniwa kwa kutumia kisingizio hicho kufanya jinai zaidi dhidi ya Wapalestina.