
Wiki iliyopita, kulikuwa na mjadala kuhusu uwiano wa mzunguko wa fedha nchini, ambapo fedha zenye thamani kubwa manthalani noti zenye thamani ya Sh10,000 na Sh5,000 zinaonekana kuzidi zile zenye thamani ndogo kama vile Sh 500, 1,000, na 2,000.
Hili ni suala ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara na limejadiliwa hapa kwenye safu yetu ya Fedha na Uwekezaji. Ukosefu huu wa fedha ndogo una athari kubwa kwa mwananchi wa kawaida na uchumi kwa ujumla.
Ukosefu wa mzunguko kwa fedha zenye thamani ndogo unasababisha ukosefu wa chenji ambao umekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara na wanunuzi. Bei za bidhaa na huduma zimeathirika, na mara nyingi wateja hulazimika kulipa zaidi ya bei halisi kutokana na ugumu wa kupata chenji.
Vilevile, inachukua muda kutoa huduma na hii inaonekana kwenye malipo ya kwenye vyombo vya usafiri na hata bidhaa mbalimbali madukani na kwenye masoko ya vyakula.
Ukosefu wa fedha ndogo, pia, unazorotesha mzunguko wa fedha. Watu wengi hukosa chenji na hivyo kushindwa kufanya ununuzi madogo madogo, ambayo kwa jumla huchangia pakubwa katika uchumi.
Hali hii inasababisha fedha kukaa mikononi mwa watu kwa muda mrefu zaidi, na hivyo kupunguza kasi ya mzunguko wa fedha.
Ili kukabiliana na tatizo hili, hatua kadhaa zinaweza kuchukuliwa kwa Benki Kuu pamoja na watumiaji wa fedha:
Mosi, utafiti wa mzunguko wa fedha. Serikali na taasisi za kifedha zinapaswa kufanya tafiti za mara kwa mara ili kuelewa mzunguko wa fedha na kubaini sababu za ukosefu wa fedha ndogo.
Pili, kutoweka akiba ya sarafu. Wananchi wanapaswa kuepuka kuweka akiba ya sarafu nyumbani. Badala yake, wanapaswa kuzitumia katika mzunguko wa kawaida wa kibiashara. Fedha haipaswi kuwa inawekwa nyumbani au kwenye kibubu. Inapaswa kuwa kwenye mzunguko.
Tatu, uwekezaji kidigitali. Kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidigitali kunaweza kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa chenji.
Kwa mfano kwa kutumia “Hisa Kiganjani” mwananchi anaweza kuwekeza fedha zake hata zenye thamani ya chini ya Sh10,000 na hivyo kuepuka kuweka fedha kwenye ‘kibubu’ au kutumia huduma za uwekeji wa akiba wa kimtandao ambazo zinatolea na mabenki kwa kushirikia na watoa huduma za simu za mkononi.
Nne, matumizi ya malipo ya kimtandao. Serikali na taasisi za kifedha zinapaswa kuwekeza katika miundombinu ya malipo ya kimtandao na kutoa elimu kwa umma kuhusu faida za matumizi ya malipo ya kimtandao.
Uwekezaji unatakiwa kuwa wa gharama nafuu kwa watumiaji. Wananchi wanapaswa kukubali kuwa malipo ya kimtandao ni sawa kabisa na kufanya malipo ya fedha taslimu.
Tano, mashine za fedha za kibenki (ATMs): Benki zinapaswa kuhakikisha kuwa ATMs zao zinatoa fedha zenye thamani tofauti, ikiwa ni pamoja na fedha ndogo. Ni kawaida ukienda kwenye ATMs iwe kwenye miji mikubwa au midogo unakuta zipo noti za Sh10,000 tu.
Sita, mashine za kutoa chenji. Ni wakati mwafaka wa kufikiria kuweka mashine za kutoa chenji kwenye sehemu za ATM za benki ama kwenye maduka makubwa ili kusaidia wananchi kupata chenji kwa urahisi.
Kwa kuchukua hatua hizi, tunaweza kupunguza tatizo la ukosefu wa fedha ndogo na kuboresha mzunguko wa fedha nchini, na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.