Dodoma. Kuongezeka kwa wimbi la matumizi ya shisha na michezo ya kubashiri maarufu ‘kubeti’ kwa vijana kumeistua Serikali na kuanza kupitia upya kwa baadhi ya sheria.
Mbali na hilo, kutokana na wingi wa talaka Serikali imetoa wito kwa viongozi waliopewa dhamana ya kufungisha ndoa, wazazi na walezi kuendelea kutoa elimu ya maadili kwa wanandoa.
Hayo yameelezwa bungeni leo Jumatano, Aprili 30, 2025 na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Damas Ndumbaro wakati akiwasilisha makadirio ya mapato ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Dk Ndumbaro ameliomba Bunge limuidhinishie Sh687.69 bilioni huku Sh162.23 bilioni zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo ni ongezeko la Sh246.43 bilioni ya bajeti ya mwaka 2024/25 iliyokuwa ni Sh441.26 bilioni huku bajeti ya miradi ya maendeleo pia ikiongezeka kwa Sh56.6 bilioni.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro na Naibu waziri wake, Jumanne Sagini wakipokea maoni ya wabunge kwenye hotuba ya bajeti ya wizara ya katiba na Sheria bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Akizungumza bungeni Dk Ndumbaro amesema kutokana na kuongezeka kwa wimbi la matumizi ya shisha, athari za kiafya zinaweza kutokana na matumizi ya bidhaa hiyo hasa kwa upande wa vijana, hivyo Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inafanya mapitio ya mfumo wa sheria zinazosimamia matumizi ya bidhaa za tumbaku.
Amesema lengo la kuishauri Serikali kuhusu namna bora ya kudhibiti matumizi ya shisha ni kulinda afya za Watanzania hasa vijana.
“Andiko la majadiliano limeshaandaliwa na hatua inayofuata ni ukusanyaji wa maoni ya wadau. Taarifa ya Mapitio ya Mfumo wa Sheria tajwa itakamilika mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema Dk Ndumbaro.
Wakati biashara hiyo iliyoanza nchini mwaka 2016 ikiendelea, baadhi ya viongozi wa Serikali walishapiga marufuku kilevi hicho kwa lengo la kuwaokoa vijana ambao ni nguvu kazi la Taifa.
Viongozi hao ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na waliokuwa wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Jordan Rugimbana (Dodoma) waliopiga marufuku matumishi ya shisha katika maeneo yao kati ya miaka ya 2016 na 2017.
“Shisha ni dawa za kulevya, ina athari kubwa kwa maisha ya binadamu, kuanzia leo (miaka iliyopita) marufuku uvutaji shisha mkoani hapa, hasa kwenye hoteli huwa wanapenda kuweka kilevi hicho,” alisema Rugimbana.

Lakini pia Juni 25, 2023, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, (DECA), Aretas Lyimo alisema ongezeko la kilevi cha shisha nchini linachochea matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza katika maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya duniani jijini Arusha, Kamishna Jenerali Lyimo alisema wamebaini baadhi ya wauzaji wa shisha kuchanganya dawa za kulevya jambo ambalo limeongeza matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Michezo ya kubahatisha
Akizungumza leo, kuhusu michezo ya kubahatisha, Dk Ndumbaro amesema Tume ya Kurekebisha Sheria imefanya tathmini ya utekelezaji wa sheria zinazosimamia michezo ya kubahatisha, Sura ya 41, ili kubaini kama malengo ya kutungwa kwa sheria hiyo yamefikiwa.
“Tathmini hii imejikita katika kuangalia ni kwa kiasi gani utekelezaji wa sheria unalinda washiriki wa michezo ya kubahatisha wasiathirike na uraibu,” amesema Dk Ndumbaro.

Amesema lengo ni kuangalia ikiwa utekelezaji wa sheria hii umeweza kulinda watoto chini ya miaka 18, wasishiriki katika michezo ya kubahatisha na kupata uraibu wa kushiriki michezo hiyo.
Amesema taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41 itakamilika kabla au ifikapo Juni, 2025.
Kubeti imekuwa ikilalamikiwa kuwa ni janga kubwa kwa vijana wa mitaani na walio vyuoni ambapo wanafunzi wa vyuoni wamekuwa ni wateja wazuri wa kamari kwa aina mbalimbali ikiwamo kubashiriki matokeo ya michezo hususan soka, mashine maarufu mchina na hata mchezo wa ‘pool table.’
Hali hiyo imewafanya vijana kupoteza muda mwingi katika kutandika mkeka wa ushindi na pia kutumia muda wa kutosha ili kufuatilia taarifa badala ya kufanya shughuli za uzalishaji.
Novemba 11, 2023, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii (Taswo) Dustan Haule alisema kwa sasa si vijana pekee wanaoshiriki kwenye michezo hiyo bali na watu wazima ambao huwaongezea msongo wa mawazo.
“Siku hizi hadi watu wazima wapo wengine wastaafu kabisa wanacheza kamari. Vijana kinachowasukuma huko ni uvivu wa kufanya kazi lakini wanatamani maisha mazuri, hivyo wanaona kamari ndiyo njia ya mkato ya kuwa milionea,”alisema.
Alisema kinachotokea badala ya kupata fedha wanajikuta wanatumia fedha na muda mwingi kucheza kamari inayowafanya washindwe kufanya shughuli nyingine na waliooa wanashindwa kuhudumia familia kutokana na changamoto ya kamari.
Ongezeko la talaka
Dk Ndumbaro amesema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umesajili na kutoa vyeti 675 vya talaka sawa na asilimia 116 ya lengo la kusajili talaka 583.
“Natoa wito kwa viongozi wote waliopewa dhamana ya kufungisha ndoa, wazazi na walezi kuendelea kutoa elimu ya maadili kwa wanandoa,” amesema.

Amesema ametoa wito kwa wanandoa kujenga utamaduni wa kuvumiliana na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia ya majadiliano ili kupunguza talaka zinazoathiri malezi ya watoto kwa mustakabali wa haki zao.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2024, kilichotolewa na Wizara ya Fedha kinaonesha kuwa ndoa zilizosajiliwa zilipungua kwa asilimia 10.89 mwaka 2023 huku talaka zilizosajiwa zikiongezeka kwa asilimia 93.7 kutoka zilizokuwepo mwaka 2022.
Wabunge wazungumza
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama ameshauri Rita chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ianze utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usajili wa ndoa zilizofungwa kidini na kimila na taratibu za usajili wa talaka nchini.
“Kutosajiliwa kwa ndoa za kimila na talaka kwa mujibu wa sheria, kutokana na elimu ndogo na mwamko hafifu kwa wananchi, kunafifisha azma ya Rita kuwa na taarifa sahihi na halisi za ndoa zilizofungwa kimila na matukio ya talaka,”amesema.
Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Shamsi Vuai Nahodha ameonesha wasiwasi kwa Watanzania kutonufaika katika miradi ya Liganga na Mchuchuma.
Hata hivyo ameonesha shaka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ofisi yake inawatumishi wanaotakiwa kuongezewa ujuzi.
“Miradi ya Liganga na Mchuchuma nilianza kusikia taarifa zake mwaka 2013 nikiwa waziri hadi leo makubaliano ya mikataba yake haijakamilika, wenzetu wanakwenda kwa utafiti wa vitu vingine kwa hiyo tutaachiwa yabaki chini kama makumbusho,” amesema Nahodha.
Ametaja makaa ya mawe kwamba dunia ipo katika uchunguzi kuhusu matumizi ya nishati safi na ukikamilika makaa yatakosa soko pia.
“Kuna umakini katika kuandaa mikataba lakini kuna hali ya kuchalewesha mikataba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipeleke vijana nje wakajifunze masuala ya mikataba kwa vitendo ili waje kutusadia,” amesema.