Ateba, Mukwala waachiwa msala Morocco

SIMBA imeanza mazoezi ikiwa katika mji wa Jadida uliopo ndani ya jiji la Casablanca, Morocco ikijiandaa na pambano la kwanza la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BRS Berkane litakalopigwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane.

Mechi hiyo ya ugenini itakayopigwa kuanzia saa 4:00 usiku inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini, lakini kuna jambo ambalo mastaa wa timu hiyo akiwamo kinara wa mabao kwa sasa wa Ligi Kuu, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala na Leonel Ateba wametakiwa kukifanya mapema.

Beki wazamani wa Yanga na Toto Africans, Ladislaus Mbogo amekifuatilia kikosi cha Simba na kusema kina uwekezano mkubwa wa kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, endapo tu itacheza kwa nidhamu mbele ya RS Berkane ya Morocco, huku akiwaachia msala washambuliaji wa timu hiyo hasa, Jean Ahoua, Leonel Ateba na Steven Mukwala wenye jukumu la kufunga mabao.

Simba inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane, Jumamosi hii kuvaana na Berkane katika mechi ya kwanza ya fainali hiyo ya CAF kabla ya kurudiana wiki moja baadae Kwa Mkapa, Dar es Salaam (japo kuna taarifa huenda mechi ikahamishiwa New Amaan, Zanzibar).

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu itapigwa kuanzia saa 4 usiku na Simba tayari imeshatua Morocco ikifikia jijini Casablanca kabla ya kesho kuanza safari ya kwenda mji utakaotumika kwa pambano hilo la kihistoria kwa Wekundu wa Msimbazi.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Mwanza, Mbogo ambaye kwa sasa ni kocha na mmiliki wa kituo cha kukuza vipaji vya soka, aliipongeza Simba kwa hatua iliyofikia, akisema ni sifa kwa taifa na Watanzania kwa ujumkla na kiu ya kila mmoja ni kutaka kuona safari hii taji linabebwa na klabu hiyo.

Mbogo amesema ameifutilia Simba kwa msimu huu na kugundua imekuwa ikisumbuliwa na tatizo la umaliziaji wa nafasi inazozitengenezwa, ambapo washambuliaji, Stephen Mukwala na Lionel Ateba wamekuwa wakifanya makosa mengi, jambo alililowataka safari hii kutoyarudia katika mechi hizo.

“Naamini kocha amefanyia kazi kuanzia safu ya ulinzi wasitengeneze nafasi za makosa, ikitokea nafasi ambayo wameitengeneza kwa ajili ya kufunga basi wafunge kwa sababu Simba wanapoteza sana nafasi mastraika mara nyingi wanapata nafasi za kufunga na hawazitendei haki,” ameisema Mbogo na kuongeza; “Mechi ya kushinda mabao matatu au manne, Simba imekuwa ikishinda moja na kama itafanya makosa, huenda ikawa mechi ngumu. Hivyo wanasisitiza tu mastraika wa timu hiyo, kwamba nafasi yoyote watakayoipata waitumie ili wachukue ubingwa, Simba ni timu nzuri imetimia kuanzia golini, mabeki hadi washambuliaji.”

Amesema mechi hiyo inazikutanisha timu kubwa mbili na kwa maoni yake RS Berkane ndio yenye hofu zaidi kuliko Simba, hivyo wachezaji wa Wekundu hawapaswi kutetemeka wakiwa ugenini bali wacheze kwa tahadhari na nidhamu ya kuwaheshimu kwani wana faida ya kumalizia nyumbani.

“Ni mechi ambayo wachezaji wa Simba wanatakiwa wafunge mkanda kweli kutokana na kila timu kuhitaji matokeo nyumbani kwake kunaweza kuwa na figisu, hivyo wajiandae kisaikolojia ni vitu ambavyo wanaweza kukutana navyo waamini kabisa vipo na vinaweza kutokea,” alisema Mbogo na kuongeza;

“Wachezaji wakienda wamejaa kwamba sisi ni wakubwa inaweza kuwagharimu kwa sababu ukishajiamini kupita kiasi unaweza ukaadhibiwa, mimi naamini kabisa ile timu inaihofia Simba kuliko Simba kuwahofia wale jamaa kwa sababu wanajua Simba ni timu ya aina gani.”

Simba inakutana na Berkane huku wenyeji wakiwa na rekodi tamu kwa mechi za nyumbani, kwani imecheza sita na imeshinda zote, ikifunga jumla ya mabao 18 bila kuruhusu bao, lakini Simba nayo imekuwa na mwenendo mzuri kwa michezo ya ugenini ya CAF kwa msimu huu kulinganisha na misimu mingine, kwani imeshinda moja, sare tatu na kupoteza mbili tu tangu raundi ya kwanza hadi kufika fainali hizo inazozicheza kwa mara ya kwanza tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 2004.

Hata hivyo, Simba imewahi kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, michuano iliyokuja kuunganishwa na ile ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho ambalo Yanga misimu miwili iliyopita ilifika fainali na kupoteza kwa bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 2-2 na USM Alger ya Algeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *