Askofu Malasusa awaita kanisani watia nia uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa vikiendelea na maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malalusa amewafungulia milango watia nia kwenda kanisani kuombewa.

Akizungumza leo Aprili 20, 2025 katika Usharika wa Azania Front wakati wa ibada ya Pasaka, amesema kanisa linafurahi washarika wake wakishiriki kwenye mambo ya kijamii, ukiwamo uchaguzi.

Kauli ya Askofu Malasusa imetolewa ikiwa imesalia miezi sita kabla ya Tanzania kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na Tume, Serikali na vyama vya siasa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi huo.

Katika ibada hiyo, Askofu Malasusa amesema kama wanajamii, Wakristo wana haki ya kupiga kura au kupigiwa kura utakapofika wakati wa uchaguzi, hivyo kushiriki kwao kwenye mchakato huo isiwe kwa kujificha.

“Wanaotaka kutia nia njooni kanisani tutawaombea, Mungu awaongoze katika safari hiyo. Kama una wito basi njoo uombewe ili Mungu akuwezeshe kutafakari,” amesema.

Pia, amewasisitiza Wakristo kote nchini kuwajibika katika kutunza amani ili utulivu na mshikamano uendelee kutawala.

“Wakristo tuone wajibu wetu wa kutunza amani. Mungu anatusisitiza kutunza amani, tunapaswa kuwa mabalozi wa amani. Tunapaswa kusimama katika amani na kuleta umoja, tuwe wapatinishi.

“Ukiwa mpatanishi kama huna la kusema ni vyema ukae kimya kuliko kusema yatakayoingiza watu kwenye magomvi,” amesema.

Katika mahubiri wakati wa ibada hiyo amewakumbusha waumini umuhimu wa kutafakari kufufuka kwa Yesu Kristo na namna ufufuo huo ulivyoleta mabadiliko kwenye maisha yao.

“Hatuna sababu ya kusherehekea Pasaka ambayo haigusi maisha yetu. Tusiruhusu chuki, ubaguzi katikati yetu, kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kumruhusu shetani kwenye maisha yetu.

“Pasaka inatuletea uhakika wa imani yetu, ni lazima tujitathmini kama tunayo furaha mpya. Je, imani yako imeimarika? Tukumbuke furaha ya kweli ni ufufuo wa Yesu kristo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *