Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Menonite Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Gabriel Magwega amesema wanawake wote wamepewa maajabu matano ya kiutawala yatakayoinua familia na Taifa au kuangusha, ikiwa hayatatumika ipasavyo.
Kiongozi huyo wa kiroho ameyataja mambo hayo kuwa mwanamke amepewa talanta ya ulinzi wa vitu mbalimbali ambavyo ni mume, familia na Taifa, mwanamke amepewa funguo katika familia na kibali cha kuombea amani, upendo na maendeleo kwa ngazi ya Taifa.
”Wanawake kwenye Taifa wamepewa mamlaka ya ulinzi wa Taifa na uwezo wa kutambua ni wapi tumetoka na wapi tunaenda kama Taifa,” amesema.

Mengine ni mwanamke amepewa fursa ya kujenga au kuharibu na ameumbiwa nguvu na uwezo wa ushawishi bila kutumia vifaa vya kivita.
“Mwanamke amewekwa kuwa kiunganishi cha familia, wamepewa uwezo wa kuvuta matokeo kwa maombi katika familia na Taifa,” amesema.
Askofu Magwega amesema hayo leo Ijumaa Machi 7, 2025 wakati wa mahubiri yake katika siku ya maombi ya dunia yaliyofanywa na Umoja wa Wanawake wa Makanisa ya Kikristo Dar es Salaam (UWAMACDA) Mkoa wa Dar es Salaam.
Mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo iliyofanyikia viwanja vya Mnazi Mmoja alikuwa ni Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson.
Askofu huyo anasema yote hayo mwanamke amepewa na Mungu na inategemea atatumiaje maajabu hayo, ili yakawe baraka katika Taifa na kuwa maajabu hayo, ndiyo humtofautisha mwanamke na mwanaume.
Amesema mwanamke kuitwa msaidizi haikufanyi uwe mnyonge na haimaanishi wewe ni dhaifu.
Sambamba na hayo, Askofu Magwega amesisitiza upendo baina ya wanawake katika ngazi zote na kuwa mshikamano ungekuwepo, kungekuwa na mabadiliko katika jamii kutokana na idadi kubwa ya wanawake duniani kote.
Alichokisema Askofu Malasusa
Aidha, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa amekumbusha kusanyiko hilo kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu na kushiriki katika hatua kwa hatua katika ngazi zote.
“Wenye wito wa kugombea nafasi zozote wasisite kufanya hivyo, ikiwa wana vigezo vyote vinavyotakiwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi,” amesema.
Malasusa ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani ametumia nafasi hiyo kulikumbusha Taifa kuwa uchaguzi ni jambo la amani na si vita.
“Tukumbuke pia kuombea hali ya hewa ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, mvua zinyeshe,” amesema.
Askofu Malasusa amesema utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ili kupunguza hatari na balaa la ukame nchini.
‘Mwanamke ni jeshi’
Katika salamu zake, Dk Tuliaamesisitiza upendo na amani kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025 ili demokrasia itendeke.
“Vitabu vya dini vimesisitiza mwanamke ni jeshi na kazi ya jeshi ni ulinzi na hakuna mlinzi dhaifu, nafasi hii ya mwanamke itumike katika kuliombea Taifa, kulinda amani na kudumisha upendo hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu,” amesema.

Dk Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM) amesisitiza Taifa kuepuka makwazo na kuwa ustawi wa maisha, ndani ya nchi hutegemea na amani iliyopo.
“Tutakapo kosa amani kipindi cha uchaguzi na kukawa na machafuko nchi itakosa amani na ustawi wa Taifa utachelewa,” amesema.
Kiongozi huyo wa Bunge amewataka wanawake kutumia siku hiyo kuzikumbuka nchi zinazopitia machafuko na changamoto mbalimbali.
Sambamba na hilo, Dk Tulia amewaasa waumini hao kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura, kuboresha daftari la wapigakura na kugombea nafasi mbalimbali ambazo wanawito nazo ili kuleta chachu ya maendeleo katika Taifa.
Awali, siku ya maombi ya Dunia (World Day of Prayer) ni tukio la kimataifa lenye lengo la kutengeneza umoja katika maombi na huduma kwa ajili ya ulimwengu.
Kihistori siku ya maombi ya dunia ilianza mwaka 1887, ambapo kundi la wanawake wa Kikristo likiongozwa na Mary Ellen James kutoka Marekani, walikusanyika ili kuanzisha maombi ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya kiroho na kijamii.
Baada ya maombi hayo kufanikiwa kwa mara ya kwanza, wazo hili lilienea haraka na kuwa na umaarufu mkubwa katika makanisa ya Kikristo duniani.
Wazo hilo lililenga kuanzisha siku maalumu ya wanawake wa Kikristo kutoka kila kona ya dunia kukusanyika ili kuombea na kutetea masuala ya haki, amani, na maendeleo.