
Dar es Salaam. Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limesema askari wake wawili wamefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa wakitekeleza majukumu ya ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili Februari 2, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda.
“Kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliyofanywa na waasi wa M23 Januari 24 na 28, 2025, JWTZ limewapoteza askari wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma.
“Taratibu za kuisafirisha miili ya marehemu wetu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mwenyezi Mungu awape uponyaji wa haraka majeruhi wetu na aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, amina,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa vikundi vya JWTZ vilivyopo nchini DRC vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC.
JWTZ inaendelea kulinda amani kwa Mwamvuli wa SADC huko Mashariki mwa nchi ya DRC (SAMDRC) eneo ambalo limekumbwa na mgogoro uliozua mashambulizi kati ya waasi wa M23 wanaopambana na Jeshi la DRC (FARDC).