Askari wapatao 40 wauawa katika shambulio kwenye kambi ya jeshi nchini Chad

Wanajeshi wapatao 40 wameuawa katika shambulizi ldhidi ya kambi ya jeshi katika eneo la Ziwa Chad. Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya rais wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mahamat Idriss Deby ameliamuru jeshi kuanzisha oparesheni ya kuwasaka washambuliaji hao, ingawa taarifa hiyo haikutaja kundi lililohusika na shambulio hilo.

Eneo la ziwa Chad limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na waasi wakiwemo wa kundi la ISIL la Afrika Magharibi na Boko Haram, ambalo liliibuka kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2009 na kuenea hadi magharibi mwa Chad.

Chad ni mshirika mkuu na  muhimu wa vikosi vya majeshi ya Ufaransa na Marekani vinavyodai kuwa vinapambana na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel, ambalo limekuwa kitovu cha ugaidi duniani unaoendeshwa na makundi matiifu kwa al Qaeda na ISIL.

Wakati huo huo Mali, Niger na Burkina Faso zimehitimisha oparesheni za kijeshi za kupambana na makundi ya kigaidi zilizokuwa zikitekeleza katika miaka ya karibuni kwa kushirikiana na Marekani na Ufaransa na badala yake zimegeukia upande wa Russia kwa msaada zaidi.