Askari wa Uingereza katika jeshi la Israel: Wapiganaji wa Hizbullah ndio bora zaidi

Gazeti la The Times limefichua kuwa Waingereza wanapigana pamoja na jeshi la Israel katika vita vya utawala huo dhidi ya Hizbullah nchini Lebanon.

Gazeti hilo limeripoti kuwa askari wa akiba wa kikosi cha miavuli wa Uingereza alirekodi kumbukumbu zake na kile kamera yake ya video ilinasa wakati wa siku 8 alizoishi baina ya uhai na kifo akipigana na jeshi la Israel huko Lebanon.

Gazeti hilo la Uingereza limeripoti kuwa, mwanajeshi huyo amedai katika kumbukumbu zake alizoziandika wakati wa likizo yake ya siku tatu na mkewe na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi 15, kwamba wengi kati ya wapiganaji wa Hizbullah aliokabiliana nao wamepata mafunzo nchini Iran na wamepata uzoefu wa mapigano nchini Syria, akiwataja kuwa “ndio wapiganaji bora kuliko wote.”

Mwanajeshi wa Hizbullah

Askari huyo Mwingereza aliyetajwa kwa jina moja la Yossi, alikuwa miongoni mwa wanajeshi walioivamia Lebanon tarehe 20 Oktoba. Gazeti la Times limefichua kuwa, brigedi mbili – kila moja ikiwa na hadi askari elfu mbili – ziliamriwa kuvamia mji wa karibu na mpaka na kusaka kile ilichodaiwa ni njia za kuingia kwenye mahandaki na ghala za silaha zilizofichwa chini ya mabanda ya kuku, kuzikwa kwenye mashamba ya mizeituni, au kupachikwa kwenye misingi ya majengo.

Karibu wanajeshi mia moja wa Israel wameuawa tangu utawala huo ulipovamia maeneo ya mpakani ya Lebanon mwezi Oktoba mwaka huu.