Askari wa uhifadhi watakiwa kuepuka migogoro na wananchi

Mwanza. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula amewaagiza askari wa Jeshi la Uhifadhi kuzingatia sera ya ujirani mwema wanapotekeleza majukumu yao, kuepuka migogoro na wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi.

Akizindua Bodi ya Magavana ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza leo Ijumaa Aprili 4, 2025, amesema kazi ya Jeshi la Uhifadhi ni kulinda rasilimali za maliasili ya Taifa kwa niaba ya umma wa Watanzania, hivyo hakuna sababu ya kuibua migogoro wala kuwaonea wananchi wanapotimiza majukumu yao.

“Jeshi la Uhifadhi linatakiwa kufanya kazi kwa kuakisi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulinda na kuhifadhi maliasili za Taifa katika mazingira rafiki na wananchi wanaoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa,” amesema Kitandula.

Ili kufikia lengo hilo, ameiagiza bodi hiyo kuhakikisha askari wa Jeshi la Uhifadhi wanaohitimu chuoni hapo wanajengewa siyo tu uwezo wa kitaaluma, bali pia uzalendo kwa Taifa na uwezo wa kuishi na kufanya kazi bila kuhitilafiana na jamii inayowazunguka.

Kuhusu sekta ya utalii, ameuagiza uongozi wa chuo hicho kuanzisha kozi za mafunzo ya muda mfupi katika nyanja za uhifadhi, maliasili, misitu na utalii ili kukuza uelewa wa jamii juu ya dhana ya ufanisi na maendeleo ya sekta hiyo kupitia utalii wa ndani.

Kitandula amesema Serikali itaongeza kuwekeza nguvu zaidi kwenye eneo la mafunzo ya kozi fupi na ndefu kwenye masuala ya sheria na miongozo ya sekta ya uhifadhi na utalii, kuwezesha Taifa kupata watumishi na wataalamu wenye sifa kufanya kazi katika maeneo na mazingira yote yaliyohifadhiwa.

“Juhudi hizo zitahusisha mazingira bora ya kutolea mafunzo ikiwemo vifaa vya kisasa vya kufundishia na matumizi ya teknolojia ya kisasa,” amesema Kitandula.

Mwenyekiti wa bodi hiyo,  Profesa Agnes Sirima ameahidi kuwa watasimamia kikamilifu na kwa weledi utekelezaji wa majukumu ya mafunzo yatakayowawezesha askari wa Jeshi la Uhifadhi kutimiza wajibu na majukumu yao.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula akikagua gwaride la Askari wa Jeshi la Uhifadhi alipotembelea Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.

Amesema uteuzi wao katika bodi hiyo ni deni kwao na watalilipa kwa kusimamia vema shughuli za chuo hicho ili hatimaye tija ionekane katika sekta ya uhifadhi na utalii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *