
Dar es Salaam. Utafiti mpya umeonyesha wagonjwa wengi walio na majeraha ya mifupa katika maeneo ya vijijini sawa na asilimia 68 hawafiki hospitali kutibiwa, huku wataalamu wa mifupa wakishauri tafiti zaidi eneo hilo.
Hali hiyo imetajwa kusababisha ulemavu wa muda mrefu na hata kukatwa viungo kwa baadhi ya wagonjwa, kupoteza uwezo wa kufanya kazi na kuzorota uchumi binafsi.
Akizungumzia kuhusu utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Theglobalsurgeryfoundation.com Aprili 2025, kiongozi mkuu Joost Binnerts amesema, walifanikisha utafiti huo baada ya kupewa ruhusa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Juni mwaka 2023.
Utafiti ulifanyika kwa ushirikiano na Hospitali ya Shirati KMT iliyopo mkoani Mara kwa ushirikiano wa karibu na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Bwire Chiragi.
Utafiti huo uliofanyika kuanzia Oktoba mpaka Desemba 2023 kwenye kaya katika wilaya ya Rorya, ulihusisha kaya 497 zenye jumla ya watu 2667, kwa kutumia sampuli maalumu.
Kwa mujibu wa Dk Joost, matokeo yalionyesha asilimia 95 ya wagonjwa hutafuta msaada kwa waganga wa jadi wa mifupa, huku ni asilimia 32 pekee wanaofikia huduma ya upasuaji hospitalini.
Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Dk Kennedy Nchimbi amesema tatizo ni kubwa maeneo yasiyofikika hivyo tafiti zaidi zinahitajika eneo hilo.
Amesema utafiti huo umefanywa kwa muda mfupi, “Tunaita ‘snapshot’ ni kama ukipiga picha kwa mbele, majibu yanayotoka ni picha iliyopo na huenda kuna mengi zaidi katika hiyo picha, unahitajika utafiti mkubwa zaidi.”
“Tunafanya utafiti mkubwa zaidi eneo hilo kwa kuwa tatizo lipo na kubwa. Utafiti wetu tunaufanya katika mikoa tisa, kwa sasa bado tunasubiri uwezeshaji tuweze kuukamilisha.”
Matokeo ya utafiti
Dk Joost amesema athari za tatizo hilo ni kubwa na kwamba zaidi ya nusu ya wagonjwa, waliripoti kupoteza uwezo wa kufanya kazi na asilimia 50 walipata kupungua kwa kipato, jambo linalokumbusha kuwa majeraha yasiyotibiwa huathiri si afya tu, bali pia riziki.
Amesema walibaini katika maeneo yenye uhaba wa huduma rasmi za mifupa, waganga wa jadi mara nyingi huziba pengo.
“Ingawa wanatambulika kitamaduni na ni rahisi kuwafikia, mara chache huwa na vifaa vya kutibu majeraha magumu hali inayosababisha matatizo, ulemavu wa muda mrefu na hata kukatwa viungo,” amesema Dk Joost.
Amesema utafiti huo unaonyesha haja ya haraka ya kuunganisha mifumo ya tiba za jadi na huduma rasmi, kuboresha uchunguzi wa awali wa wagonjwa na kuimarisha upatikanaji wa huduma salama na ya haraka ya upasuaji.
Utafiti ulivyofanyika
Utafiti huo mdogo ulifanyika kuhusu ukubwa wa tatizo la kuvunjika kwa viungo maeneo ya vijijini na ukweli kuhusu baadhi kufuata huduma kwa waganga wa jadi wa mifupa.
Utafiti huu ulilenga kubaini kiwango cha majeraha ya mifupa kila mwaka, athari zake na tabia ya wagonjwa katika kutafuta huduma za afya katika maeneo ya vijijini.
“Tulifanya utafiti wa kitaifa wa kaya katika wilaya ya Rorya, Tanzania tukihusisha kaya 497 zenye jumla ya watu 2667, kwa kutumia sampuli. Tuliwahoji wakuu wa kaya kuhusu upatikanaji wa huduma za mifupa na matukio ya kuvunjika kwa viungo miongoni mwa wanakaya.
“Kisha tulichagua watu wasiozidi watatu kutoka kila kaya kwa bahati nasibu ili kuwahoji. Kutokana na majibu 1448, tulikokotoa kiwango cha matukio ya kuvunjika viungo.”
Dk Joost amesema walifuatilia kwa kuuliza kuhusu huduma za afya walizotafuta na kuthibitishwa kwa kutumia picha za radiolojia. Wagonjwa waliothibitishwa walijaza dodoso kuhusu ulemavu na athari za kifedha.
Amesema matokeo yalithibitisha radiolojia za kuvunjika kwa viungo 11 kati ya washiriki 1,448 waliojaza dodoso, sawa na asilimia 0.76 kwa mwaka.
“Majeraha mengine matano yalibainika kutoka kwa watu ambao hawakuchaguliwa, hivyo jumla ya watu waliothibitishwa walikuwa 16.
“Idadi ya waliokwenda kwa waganga wa jadi ilikuwa kubwa zaidi kuliko waliokwenda hospitalini (sawa na asilimia 95 dhidi ya asilimia 32, p < 0.0005). Asilimia 62 waliokwenda kwa waganga wa wajadi walisema ni gharama nafuu, asilimia 29 walisema ni kupona haraka.
“Asilimia 62 ya wagonjwa waliripoti kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi au walihitaji msaada wa usafiri na asilimia 50 walipata upungufu wa kipato,” amesema Dk Joost.
Amesema kiwango cha matukio ya kuvunjika kwa viungo katika utafiti huu kilikuwa asilimia 0.76 kwa mwaka.