Ashanti yupo tayari kuongeza mtoto na Nelly

Marekani. Mwimbaji wa Marekani, Ashanti, 44, amesema yupo tayari kuongeza mtoto wa pilli na mpenzi wake wa siku nyingi, Nelly, 50, ikiwa ni takribani miezi sita tangu ajifungue mtoto wao kwanza na kumpa jina la la Kareem Kenkaide (KK).

Hata hivyo, Ashanti aliyeshirikiana na Nelly katika kibao chao, Body on Me (2008), alikiri kuwa anatamani awamu hii apate mtoto wa kike maana nyumba yake imejaa wanaume huku akieleza jinsi hatua ya kuwa mama ilivyombadilisha.

Ikumbukwe wawili hao walianzisha uhusiano mwaka 2003 baada ya kukutana katika tuzo za Grammy, walidumu hadi mwaka 2013 na kuachana ikiwa ni miaka 10 ya penzi lao, lakini miaka 10 baadaye, yaani 2023 wakarudiana na kuanzisha familia.

Agosti 2024 ndipo Ashanti alijifungua mtoto wake wa kwanza ila kwa upande wa Nelly huyo ni wa tatu maana katika mahusiano yake mengine alishapata watato wawili, Chanelle na Cornell huku akiasili watoto wawili wa dada yake, Jaqueline aliyefariki 2005.

“Tunaenda kuongeza mtoto mwingine, kwa hakika nataka msichana wa kuweka mizani sawa maana nyumbani nimezidiwa, kwa hivyo kupata msichana litakuwa jambo zuri,” alisema Ashanti wakati akiongea na E! News.

Utakumbuka Ashanti ni mwanamuziki wa kwanza wa kike duniani kushika namba moja na mbili katika chati ya Billboard Hot 100, ni kupitia wimbo wake, Foolish (2002) na What’s Luv? (2002) alioshirikishwa na Fat Joe.

Akizungumzia hatua ya kuwa mama kwa jumla, Ashante alisema, “Ninahisi msisimko wa ajabu, kufurahishwa sana, na kuwa mwenye unyenyekevu. Maisha yangu yamebadilika kabisa na kuwa bora. Ninahisi kutosheka, unajua?, kikombe changu kimejaa,”.

Hii si mara yake ya kwanza kuzungumzia jinsi kuwa mama kumebadili maisha yake na hata kumeathiri kazi yake ya uigizaji. Kwa sasa anaigiza katika filamu ijayo ya ‘No Address’ akiwa na William Baldwin ambapo anacheza kama mkongwe asiye na makazi.

“Kuwa na mtoto kunakuza upendo na utu ambao mtu anakuwa nao. Na, wakati mwingine mimi hushukuru sana mama yangu, binamu, shangazi, na familia kwa kuwa nami kwa kipindi  chote,” alisema.

Pia alieleza jinsi inavyomfanya atake kusaidia wengine zaidi hata kuliko hapo awali, alisema, “Sasa hivi mimi ni kama, ni nini kingine tunaweza kufanya?. Je, tunaweza kushirikiana?, kuna nguo chapa hapa, tunaweza kufua pamoja? Ndivyo tunaishi wakati huu,”.

Ikumbukwe Ashanti alifanya vizuri kimuziki baada ya kusainiwa katika lebo ya Murder Inc Records na kutoa albamu yake ya kwanza, Ashanti (2002) iliyoshinda tuzo ya Grammy 2003.

Naye mpenzi wake, Nelly alipata umaarufu zaidi duniani baada ya kuachia wimbo wake, Dilemma (2002) akimshirikisha Kelly Rowland kutoka katika albamu yake ya pili, Nellyville (2002) iliyotoka chini ya Universal Records na Fo’ Reel Entertainment.

Kwa mujibu wa Chama cha Rekodi za Muziki Marekani (RIAA), hadi Machi 2011, albamu ya Nellyville ilikuwa imegonga Platnum mara sita ikiuza nakala zaidi ya milioni 6.4 Marekani ikiwa ni albamu ya 14 ya rap kuuza zaidi nchini humo kwa muda wote.