
Dar es Salaam. Wakati mashabiki wa Simba wakisubiria kwa hamu droo ya mechi za robo fainali za Kombe la Shirikisho Afrika ili kujua timu yao itapangwa na nani kuitafuta nusu fainali, kocha wa Asec Mimosas ya Ivory Coast Mfaransa Julie Chevalier amesema hatamani timu yake ikutane na Mnyama.
Asec pamoja na Stallenbosch ya Afrika Kusini na Al Masry ya Misri zilizomaliza nafasi ya pili katika makundi ya B, C na D, ni kati ya timu zinazoweza kukutana na Simba iliyomaliza kinara wa Kundi A.
Akizungumza na Mwananchi Chevalier, amesema hatamani kabisa kukutana na Simba katika hatua hiyo, kutokana na kujua mziki kila wanapokutana nao hasa kwa mechi za Kwa Mkapa.
Rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimewahi kukutana mara sita katika michuano tofauti ya CAF, ikiwamo mara mbili katika Kombe la Shirikisho na nne za Ligi ya Mabingwa, huku kila moja ikishinda mara mbili na nyingine mbili kumalizika kwa sare, mechi zote sita zikiwa ni za hatua ya makundi.
Safari hii kuna uwezekano wa kukutana tena katika Kombe la Shirikisho, lakini ni hatua ya robo fainali na Kocha Julie alisema moja kati ya kitu ambacho hakitamani hatua inayofuata ni kukutana na wapinzani wao hao.
“Simba ni timu kubwa nimeiona msimu huu, pia nimewahi kucheza nayo, haina utani kabisa katika michuano ya kimataifa. Ina kikosi hatari wala siyo cha kukibeza ukikutana nacho ni lazima ujipange vilivyo kwani ukicheza vibaya atakupiga ugenini na nyumbani,” alisema Julie na kuongeza;
“Kilichoongezeka msimu huu kwa Simba ni mastaa wakali wanaokifanya kikosi hicho kuwa kipana zaidi, pia kocha wake ni mpya na falsafa zake ni kubwa.”
Alisema kati ya timu tatu kati ya nne zilizoongoza makundi ya michuano ya msimu huu, ikiwamo watetezi, Zamalek na RS Berkane pamoja Simba, anaona ni heri akutane na timu hizo nyingine na sio Mnyama kwani wanaujua mziki wake Kwa Mkapa, pia ni timu yenye uzoefu na mechi kubwa za maamuzi.
“Kuna Zamalek na Berkane, kwangu mimi bora timu moja kati ya hizi na siyo Simba, tumewahi kucheza nao kwa Mkapa, tunajua walivyo.”
Hata hivyo, licha ya kauli hizo bado Simba haipaswi kubweteka kwani Asec ambayo imekuwa ikizalisha mastaa kadhaa wakubwa imekuwa na matokeo mazuri ikiwa nyumbani dhidi ya Simba, kwa kutopoteza na mara ya mwisho msimu uliopita ilitoka suluhu, baada ya awali kutoka sare ya 1-1 Kwa Mkapa.
Katika mechi mbili za nyumbani Asec imeifunga Simba kwa 3-0 na 4-3, wakati ilipoteza ugenini mbele ya Mnyama kwa wa 3-1 na 1-0 ikiwa ni wastani mzuri wa mabao kwani imevuna mabao tisa dhidi ya saba katika mechi hizo sita zilizochezwa 2003, 2022, 2023 na 2024.
Huu ni msimu wa sita kati ya saba Simba inafanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF ikiwa ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye mashindano kwa sasa