
Tanga. Jumla ya asasi 157 za kiraia zimepewa kibali na Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajali ya kutoa elimu ya mpigakura katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele ametoa taarifa hiyo leo Jumapili Februari 2, 2025 wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa waratibu wa uandikishaji, maofisa waandikishaji, maofisa waandikishaji wasaidizi wa ngazi ya jimbo, maofisa uchaguzi, maofisa ugavi na maofisa Tehama wa halmashauri zilizopo mkoani Tanga.
Amesema Tume hiyo pia imetoa vibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika uboreshaji wa daftari hilo, ambapo kati ya hizo tisa ni za kimataifa.
Mwenyekiti huyo amewataka maofisa waandikishaji nchini kote kutoa ushirikiano kwa waangalizi hao mara wanapokwenda kwenye maeneo yao, kwani ni wadau muhimu katika hatua hiyo.
“Nasisitiza kwa maofisa waandikishaji kuwa wanapofika katika maeneo yao, wapewe ushirikiano kwa kuwa ni wadau muhimu, vitambulisho watakavyokuwa navyo walivyopatiwa na Tume ni utambulisho tosha,” amesema Jaji Mwambegele.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhani amewahimiza waliopewa jukumu la kuendesha uboreshaji wa daftari hilo mkoani Tanga kutekeleza majukumu yao kwa umakini, ikiwamo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa na vinategemewa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini.
“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutasababisha athari kubwa katika ukamilishaji wa hatua hiyo muhimu,” ameelekeza Kailima.
Daudi Jumanne mkazi wa mtaa wa Kange jijini Tanga, ameishauri Tume kutumia vyombo vya habari, matangazo kupitia vipeperushi na wasanii mbalimbali katika kuwahamasisha watu kujitokeza kujiandikisha, kwani anaamini wengi ama hawajajiandikisha au wamepoteza vitambulisho.
Hatua ya uboreshaji daftari hilo kwa mkoa wa Tanga, inatarajiwa kuanza Februari 13 na kufikia tamati Februari 19 mwaka huu.