
London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ameomba ushauri kwa mastaa wake wa Arsenal kusema ni straika gani wanataka asajiliwe kabla ya dirisha hili la Januari halijafungwa.
Arsenal ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolves jana na kuendelea kuonyesha upinzani mkali kwenye msimamo wa Ligi Kuu England sasa ikiwa tofauti ya pointi sita tuy dhidi ya Liverpool iliyoibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Ipswich Town.
Arsenal inatafuta ya kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji katika dirisha hili la Januari baada ya kikosi chao kuandamwa na wachezaji wengi wenye majeruhi kwenye eneo hilo la mbele ikiwamo Bukayo Saka na Gabriel Jesus ambao watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Lakini, sasa ikiwamo imebaki muda usizidi wiki moja kabla ya dirisha la usajili halijafungwa, Arteta anaonekana kuwa kwenye hatua za mwisho za kuleta sura mpya kwenye kikosi chake huku mchezaji anayemhitaji zaidi straika Benjamin Sesko akionekana kwamba atabaki kwenye timu yake ya Red Bull Leipzig labda kama tu kutakuwa na ofa ya maana katika dakika za mwisho.
Washika Bunduki hao wa London wamekuwa wakihusishwa pia na mastraika Alexander Isak, Dusan Vlahovic na Matheus Cunha.
Baada ya ushindi wa mabao 2-1, iliyopata Arsenal mbele ya mahasimu wao Tottenham Hotspur wiki iliyopita, kiungo wa miamba hiyo ya Emirates, Declan Rice alisema: “Tuna upungufu kiasi kwenye fowadi yetu. Sitashangaa kama tutakwenda kufanya kitu fulani kwenye dirisha hili la Januari.”
Alipoulizwa kama wachezaji wake wamezungumza naye kuhusu usajili mpya katika kuelekea mchezo wa Ligi Kuu England wa jana Jumamosi dhidi ya Wolves uwanjani Molineux, kocha Arteta alisema: “Siyo kihivyo, lakini tumekuwa tukielekea huko, tumekuwa watu wa kuangaliana.
“Tuna watu wachache sana katika baadhi ya namba na hilo limekuwa kwa wiki nyingi sana, hivyo tunatazama uwezekano wa kufanya jambo. Na ndiyo maana tunajaribu juu ya kufanya kitu sahihi kwa ajili ya klabu na timu hii ndiyo kipaumbele chetu.”
Arteta alisema siku zote amekuwa akishauriana na wachezaji wake juu ya wachezaji wapya wanaokuja kwenye timu ili kufahamu kile watakachoweza kuleta kwenye kikosi na kwenye hilo, Arteta alisema: “Hilo linatufanya sisi tuwe mbali na kompyuta na masuala ya kukusanya takwimu. Mchezaji anaweza kuwa mfungaji wa mabao mengi, lakini vipi kama mchezaji huyo atashindwa kufunga bao kwenye mechi sita au saba? Hicho ni muhimu na ndio maana unahitaji kuwa na mijadala ya mapema na wachezaji.”
Arteta amehakikishiwa maisha na wamiliki wa klabu hiyo Stan na Josh Kroenke kwamba watafanya usajili kwenye dirisha hili la Januari. Lakini, uamuzi mkubwa umebaki kwenye kutambua kile ambacho mchezaji atakileta kwenye timu kama hilo litatibua mpango wao wa mwisho wa msimu kwenye dirisha kubwa la usajili.
Kuhusu usajili wa mkopo timu hiyo imeshanasa wawili, kipa Neto kutoka Bournemouth na winga Raheem Sterling kutoka Chelsea.
Mabeki Jakub Kiwior na Oleksandr Zinchenko nao wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kuachana na Arsenal kwenye dirisha hili la Januari, ambapo Borussia Dortmund imeripotiwa kuvutiwa na huduma ya staa wa kimataifa wa Ukraine, Zinchenko.
Kama wachezaji hao wataondoka mapema, basi Arsenal itapata pesa ya kuboresha bajeti yao katika kunasa huduma ya mshambuliaji mpya kuwa pia itamkosa Myles Lewis-Skelly’ ambaye alipewa kadi nyekundu kwenye mchezo wa jana.