
Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amesikitishwa na timu yake kupita katika dirisha dogo la usajili la Januari 2025 bila kusajili mchezaji yeyote.
Kuumia kwa Gabriel Jesus na Bukayo Saka kulitegemewa kungeifanya Arsenal isajili katika dirisha la majira ya baridi lakini hilo halikutokea jambo ambalo Arteta alisema hajafurahishwa nalo.
“Tulikuwa na nia ya wazi ambayo ni siku zote dirisha linapofunguliwa, kusaka fursa za kuimarisha kikosi chetu kwa wachezaji ambao wanaweza kutipatia matokeo.
“Kwa wachezaji walio majeruhi, tumeathirika na hatujafanikiwa. Tumesikitishwa katika namna hiyo lakini pia tulikuwa makini sana kwamba tunahitaji kuleta aina fulani ya wachezaji na tulipaswa kuwa na nidhamu ya hilo pia. Nadhani ndivyo tulivyokuwa.
“Ni katika wasifu, mchezaji ambaye tunaamini anaweza kutuweka bora zaidi. Kiuchumi kuna njia nyingi, mambo mengi ambayo tunapaswa kukaa nayo kwenye mstari ambao umetufanya tuwe hapa na kuanzia hapo kujaribu kuimarika,” alisema Arteta.
Katika dirisha hilo dogo la usajili la Januari, wachezaji watatu waliondoka Arsenal ingawa wote walikuwa hawapo katika mipango ya Arteta kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Arsenal ilimpoteza beki wa kati Ayden Heaven (17) aliyetimkia Manchester United na mwingine ni Josh Robinson (20) aliyejiunga na Wigan Athletic mtawalia.
Mchezaji mwingine ambaye Arsenal ilimfungulia milango katika dirisha dogo la usajili ni Marquinhos ambaye alijiunga na Cruzeiro ya Brazil.
Katika dirisha hilo dogo, Arsenal ilitajwa kuwania saini ya mshambuliaji wa Astin Villa, Ollie Watkins lakini dau ala Pauni 40 milioni ambalo ilitoa, lilikataliwa ambapo ilitajiwa dau la Pauni 60 milioni ililoligomea.