Arteta aingiwa ubaridi ubingwa EPL

London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema ana wasiwasi kwamba injini ya kufanya kazi ili kuwawezesha kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 21 msimu huu huenda imefeli mapema.

Arsenal ambayo sasa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 11, tofauti ya alama kati yao na vinara Liverpool ni tisa hadi sasa na Gunners hawajashinda katika mechi zao nne za ligi zilizopita.

Arteta ambaye pia aliwabwatukia wachezaji wake kwa kuruhusu bao kizembe na kufanya mchezo huo umalizike kwa sare, amesema wakati ligi inaanza alijua anahitaji kuweka vitu vidogo vidogo kwenye timu yake lakini majeraha yamesababisha abadilishe vitu vingi hali ambayo anaamini inasababisha apate matokeo mabaya.

“Tulikuwa na mpango mkakati wa nini tulihitaji kufanya kama timu na lengo lilikuwa ni kurekebisha gari (timu) yetu iwe bora zaidi kwa kuiongezea vitu, lakini imekuwa tofauti na kila simu tunalazimisha kubadilisha kabisa kile tulichopanga, kuanzia injini, magurudumu au usukani kwa sababu ya majeraha.

“Hakuna kitu tunaweza kufanya kuhusu hilo. Ninachoomba ni kwamba baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa tuwe na timu ikiwa na wachezaji wote tena wenye afya njema na waweze kucheza, kwa sababu hili limekuwa tatizo letu kwa wiki nane. Tumekuwa na majeraha baada ya majeraha,” alisema Arteta.

“Nahitaji kuona timu yangu yote ikiwa kamili, kwa sababu nia ya kutaka kushinda tunayo hilo halipingiki, kwangu mimi timu inapokuwa inafanya vibaya huwa nahitaji kupambana kuonyesha nilichonacho kwa sababu ni wakati ambao kile mtu atakuwa anataka kuona unafanya nini.”

Arsenal imekuwa ikiandamwa na majeraha ya mara kwa mara katika kikosi ambapo wengi wa wachezaji wao muhimu wamekuwa wakiumia na wengine kuonyeshwa kadi nyekundu tangu kuanza kwa msimu huu jambo linalosababisha wasiwe na kikosi chao kamili kilichofanya vyema misimu miwili iliyopita.

Katika mchezo huo wa London dabi, mastaa wawili Declan Rice na Bukayo Saka walizua wasiwasi baada ya kuomba kutoka nje kutokana na maumivu.

Kapteni wao, Martin Odegaard alianza kwa mara ya kwanza baada ya kukaa nje kwa karibia miezi miwili tangu alipopata majeraha akiwa katika majukumu ya timu ya taifa.

Akizungumzia bao la kusawazisha la Chelsea lililofungwa na Pedro Neto baada ya wao kuongoza kupitia Gabriel Martinelli, Arteta alisema amesikitishwa sana kwa sababu lilifanywa kosa la kizembe.

“Nimesikitishwa sana na jinsi tulivyoruhusu bao. Ile sio aina yetu ya uzuiaji na wala sio kiwango chetu, ni wazi unapotoa nafasi na muda kwa mchezaji wao yeyote utaadhibiwa, kwahiyo, ile kwangu haikuwa bahati mbaya. Ile sio namna ya uchezaji wetu, inabidi tujilaumu wenyewe. Inapaswa tuwe makini zaidi hususani katika mechi ambazo hatufungi mabao mawili, matatu au hatufungi kabisa. Nimesikitishwa na matokeo kwa sababu naamini tulistahili zaidi ya hiki. Baada ya bao lao timu yetu ilionyesha meno yake. Tulikuwa wakali sana, tulitengeneza nafasi tatu kubwa. Kwa bahati mbaya hatukuweza kuweka mpira wavuni, lakini tulistahili kushinda.”

Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca yeye alisema matokeo hayo ni mafaniko kwake kwani timu yake bado inahitaji kujitafuta kufikia levo za Arsenal ambayo ilimaliza nafasi ya pili msimu uliopita.