London, England. Baada ya mshambuliaji wa Arsenal, Kai Havertz kupata maumivu ya misuli ya paja wakati wa mazoezi huko Dubai, mshambuliaji huyo hatacheza mechi zote zilizobaki msimu huu huku kocha Mikel Arteta akisisitiza kwamba haitaji mshambuliaji mpya kwa sasa.
Hiyo ni habari mbaya kwa Arteta katika kipindi ambacho anawakosa nyota wengine watatu wa ushambuliaji, Bukayo Saka, Gabriel Jesus na Gabriel Martinelli kutokana na majeraha.

Saka anatarajiwa kurudi uwanjani hivi karibuni kama ilivyo kwa Martinelli lakini Jesus atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima ambapo sasa ataungana na Havertz ambaye ndio amekuwa tegemeo la Arsenal msimu huu.
Kumkosa Havertz ni pigo kubwa kwa meneja wa Arsenal, Mikel Arteta kwani Mjerumani huyo ndiye amekuwa akitumika kuziba pengo la kukosekana kwa mshambuliaji wa kati, hivyo maumivu yake yanaweka shakani ndoto ya timu hiyo kutwaa mataji msimu huu.
Licha ya changamoto hizi, Mikel Arteta amesisitiza kuwa Arsenal haitasajili mshambuliaji mpya kwa sasa, bali itajikita katika kutumia wachezaji waliopo kikosini.

Wachezaji wanaotarajiwa kupewa nafasi katika safu ya ushambuliaji ni Leandro Trossard na kijana mdogo Ethan Nwaneri. Pia, Raheem Sterling, ambaye yupo Arsenal kwa mkopo kutoka Chelsea, anatarajiwa kuwa sehemu ya safu ya ushambuliaji, ingawa hajaonyesha kiwango bora tangu ajiunge, akiwa na bao moja pekee na pasi mbili za mwisho katika mechi 18.

Havertz ndiye mfungaji bora wa Arsenal msimu huu ambapo hadi sasa ameifungia mabao 15 katika mashindano tofauti msimu huu ambayo yamechangia kuifanya iwe katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na pia kuiwezesha kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ripoti zinaeleza kuwa Arsenal imepanga kufanya usajili mkubwa katika nafasi ya mshambuliaji wakati wa majira ya kiangazi huku wachezaji wawili wanaotajwa kuwa chaguo la kwanza ni Benjamin Šeško wa RB Leipzig na Alexander Isak wa Newcastle United. Mbali na mshambuliaji, Arsenal pia inapanga kusajili winga mpya ili kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao.
Arsenal kesho Jumamosi, Februari 15, 2025 itakuwa kwenye uwanja wa King Power kukabiliana na Leicester City katika mwendelezo wa Ligi Kuu England.