Arsenal imetupwa nje ya mashindano ya Kombe la Carabaobaada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Newcastle katika mchezo uliochezwa Uwanja wa St. James’ Park.
Katika mchezo wa awali uliopigwa kwenye Uwanja wa Emirates Arsenal ililala pia kwa idadi hiyo ya mabao na kuifanya itupwe nje kwa jumla ya mabao 4-0.

Mabao ya Newcastle yalifungwa na Jacob Murphy katika dakika ya 19 baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Alexander Isak. Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika Newcastle ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Zilipita dakika saba baada ya kipindi cha pili kuanza ambapo Newcastle iliandika bao la pili kupitia kwa Anthony Gordon.
Kipa wa Arsenal, David Raya alifanya kosa baada ya kupiga pasi fupi ndani ya eneo la hatari ambayo ilinaswa na Fabian Schär na kumpasia Anthony Gordon ambaye alipachika bao la pili.
Arsenal inapoteza mchezo wa tano dhidi ya Newcastle katika mashindano yote waliyokutana ikiwa chini ya kocha, Mikel Arteta nba kuonekana kuwa ni mopja ya timu inayowamudu zaidi.

Newcastle imeingia kwenye fainali ya Kombe la Carabao ikiwa inamsubiri mshindi kati ya Liverpool au Tottenham ambaye itaungana naye kucheza mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.
“Tumefanya vibaya na hakuna maneno mengine, tunakwenda kuwa na kipindi kifupi cha kujiandaa na michezo inayokuja, lakini tukubali kuwa tuna kazi kubwa ya kufanya ili kurudisha morali kwenye timu,” alisema Mikel Arteta
Huu unakuwa ni mwendelezo wa kufanya vibaya kwa timu hii katika michuano ya Carabao ikiwa ndio timu pekee kati ya zile sita kubwa zilizoshinda kombe hilo mara chache (2) licha ya kucheza fainali nane.
Mara ya mwisho timu hii kucheza fainali ya Carabao ilikuwa msimu wa 2017/18 ambapo ilichapwa mabao 3-0 na Manchester City.
Hadi sasa imepita miaka 31 tangu mara ya mwisho ichukue kombe hilo msimu wa 1992/93, tangu hapo mara kadhaa imekuwa ikiishia nusu fainali na muda mwingine hatua za awali.
Baada ya ushindi wa jana, Newcastle ambayo haijawahi kabisa kushinda kombe hili itakuwa inasubiria mshindi wa mchezo kati ya mabingwa wa kihistoria wa Carabao, Liverpool watakaoumana na Tottenham Hotspur.
Katika mchezo huo utakaopigwa Anfield, Liverpool itatakiwa kupata ushindi wa mabao mawili au zaidi kwa sababu mchezo wa mkondo wa kwanza Majogoo walichapwa bao 1-0.