Arsenal yanyimwa Ubingwa EPL

London, England. Kocha wa Arsenal Mikel Arteta, amewaambia wachezaji wake waendelee kufikiri kuhusu michezo inayofuata na kuachana na matokeo yao dhidi ya Manchester City.

Arsenal juzi ilionyesha kiwango cha juu na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Manchester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa katika Uwanja wa Emirates.

Timu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwenye ligi ilifanikiwa kwenda mapumziko ikiongoza 1-0, lakini ilirejea kipindi cha pili na kufunga mabao manne yaliyowapa ushindi huo muhimu na kuendelea kuiweka City kwenye wakati mgumu.

“Mechi hii imekwisha, lazima tuendelee kufikiri kuhusu michezo mingine inayokuja huko mbele na kuondoa mawazo hapa sasa, ulikuwa mchezo mzuri na nataka kumpongeza kila mchezaji aliyekuwa uwanjani,” alisema Arteta baada ya mchezo kumalizika.

Hata hivyo, alipoulizwa na waandishi wa habari maoni yake kuhusu aina ya ushangiliaji ya kinda wake Lewis-Skelly aliyeiga staili ya mshambuliaji wa Manchester City Earling Haaland baada ya kufunga, alisema ameiona lakini hana la kusema.

 “Sina maoni.  Nimeona jinsi ambavyo alishangilia, lakini sina jambo lolote ambalo naweza kusema kuhusu jambo hilo.

“Lazima tufikiri kuhusu sisi na kuachana na kila kitu kilichotokea, hii ni sehemu ya mchezo ndani ya uwanja, kila kitu kinachotokea pale ni sehemu ya mchezo, nafikiri tumekuwa kwenye soka kwa miaka mingi, tujaribu kuachana nalo, hakuna kitu ambacho tunaweza kufanya sasa,” alisema kocha huyo raia wa Hispania.

Ushindi huu umeifanya Arsenal iendelee kuisogelea Liverpool kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kufikisha pointi 50 zikiwa ni sita nyuma ya vinara hao ambao pia wana mchezo mmoja mkononi.

Hata hivyo, umeongeza gepu kubwa dhidi ya Man City iliyopo nafasi ya nne ambapo kwa sasa imewaacha kwa pointi tisa.

United kama kawaida

Manchester United iliendelea kuwa kwenye wakati mgumu kwenye Ligi Kuu England baada ya kulala kwa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace na kushuka hadi nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 29 baada ya michezo 24.

Ushindi wa Palace umekuwa mbaya kwa United kwa kuwa sasa timu hiyo imesogea hadi nafasi ya 12 iliyokuwa imekaa Man United ikiwa na pointi 30.

Kocha wa United Ruben Amorim, amesema timu yake haikuonyesha kiwango kizuri na sasa anapambana kwa nguvu kubwa kuhakikisha kuwa inakamilisha usajili wa mshambuliaji mmoja kabla dirisha halijafungwa leo usiku.

“Hatukucheza vizuri, huu ni ukweli na hakuna wa kuupinga, lakini tunazidi kupambana kuhakikisha kuwa tunapata mshambuliaji mmoja sokoni kabla dirisha halijafungwa ingawa ni kazi kubwa sana kufanya hivyo, tutajitahidi kuona nini kitatokea,” alisema kocha huyo ambaye mshambuliaji wake Marcus Rashford ameondoka na kujiunga na Aston Villa.