Arsenal yajiweka sawa, Spurs yapigwa

Arsenal imerudi kwenye mbio za kuwania ubingwa baada ya kuichapa Chelsea bao 1-0, huku Tottenham Hotspur wakiendelea kuwa na maisha magumu.

Ikiwa kwenye Uwanja wa Emirates Arsenal ilionyesha kiwango kizuri kipindi cha kwanza cha mchezo huo na kufanikiwa kupata bao pekee kupitia kwa Mikel Merino aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 20 ya mchezo huo uliokuwa wa kuvutia.

Kabla kufunga kwenye mchezo huu, Arsenal ambayo imefunga mabao mengi kwa kona kuliko timu zote ikiwa nayo 27 kuanzia msimu uliopita, ilikuwa imepiga kona 98 bila kufunga bao.

Timu zote zilionyesha kiwango kizuri, huku Chelsea ambayo ushindi kwenye mchezo huo ungefufua matumaini yao ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao ikipoteza nafasi kadhaa za wazi za kufunga mabao.

Hata hivyo kitendo cha kukosekana kwa mshambuliaji wao Cole Palmer kulikuwa tatizo kwao.

Palmer kabla ya mchezo huu alikuwa ndiye mchezaji aliyecheza michezo mingi zaidi ya Chelsea msimu huu, akiwa na mabao 14 na kutoa pasi sita zilizozaa mabao kwenye michezo 28 ya ligi. lakini akiwa ameshaifunga Arsenal mara mbili kwenye michezo waliyokutana.

Ushindi huu umeifanya Arsenal iendelee kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 58 ambazo ni 12 nyuma ya vinara Liverpool, huku Chelsea ikiendelea kubaki nafasi ya nne na pointi 49 ikiwa ni moja mbele ya Man City iliyopo nafasi ya tano zote zikicheza mechi tisa.

Katika mchezo mwingine, kipindi cha pili kilikuwa kibaya kwa Spurs baada ya kuruhusu mabao mawili ndani ya dakika kumi na kulala 2-0 dhidi ya Fulham.

Ushindi huu umeifanya Fulham kusogea hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku Spurs ikiendelea kuwa na wakati mgumu kwenye nafasi ya 13 ikiwa na pointi 34, ambazo ni sawa na timu iliyopo nafasi ya 16 West Ham zote zikicheza michezo 29.

Rodrigo Muniz, alianza kuifungia Fulham katika dakika ya 78 ya mchezo huo, huku dakika kumi baadaye Ryan Sessegnon ambaye aliingia muda mchache akifunga la pili kwenye mchezo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *