
London, England. Arsenal jana ilicheza mechi yake ya mwisho nyumbani kwenye Ligi Kuu England ikiwa inapewa nafasi kubwa ya kumaliza nafasi ya pili baada ya kuichapa Newcastle bao 1-0 na kufikisha pointi 71.
Huu ni msimu mwingine ambao Arsenal imemaliza bila kutwaa ubingwa wowote kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Kwa kipindi cha miaka mitano ambayo kocha Mikel Arteta amekaa kwenye timu hiyo amefanikiwa kutwaa kombe moja tu la FA huku misimu mingine akimaliza bila kombe lakini kipindi chote akipata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza jana baada ya mchezo huo uliokuwa mgumu kwa timu zote, kocha huyo raia wa Hispania alisema mabosi wa timu hiyo wanatakiwa kufanya kila linalowezekana ili timu hiyo ifanye usajili mkubwa kwenye dirisha lijalo.
Alisema anaamini kuwa wachezaji wake wanne au watano wataondoka kwenye timu hiyo hivyo ni lazima ufanyike usajili mkubwa klabu hapo.
Baadhi ya wachezaji wanaotarajiwa kuondoka Arsenal ni Jorginho, ambaye anajiunga na Flamengo ya Brazil pamoja na Kieran Tierney anayekwenda Celtics.
Wengine ni Neto anayecheza kwa mkopo, Raheem Sterling pia ataachana na Arsenal pamoja na Oleksandr Zinchenko huku Thomas Partey mkataba wake ukiwa unaelekea ukingoni.
“Ni sahihi kuwa tunahitaji wachezaji wengine klabuni kwa kuwa kikosi chetu ni kidogo sana, lakini juu ya hilo tunapoteza wachezaji wanne au watano mwishoni mwa msimu huu, wengine mikataba inamalizika na wengine kipindi cha mkopo kinaisha.
“Nafikiri bodi wanatakiwa kufanya kila wanaloweza kuhakikisha kuwa tunafanya usajili mzuri ili tuweze kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao.
“Ni vizuri kuhakikisha kuwa msimu ujao tunakuwa na wachezaji imara siyo tu kumaliza ligi sehemu nzuri, bali kuhakikisha kuwa tunatwaa ubingwa,” alisema Arteta.
Alipoulizwa anaweza kufanyaje ili timu hiyo imalize msimu ujao vizuri, Arteta alisema uwezo wake ni kuhakikisha kila kitu klabu hapo kinaenda vizuri yeye pamoja na wenzake kwenye benchi.
Msimu huu ikiwa na pointi 71, Arsenal ipo nafasi ya pili ikiwa pointi 12 nyuma ya Liverpool ambao tayari wameshatwaa ubingwa na wana mchezo mmoja mkononi, msimu uliopita Arsenal ilimaliza ya pili ikiwa nyuma ya Man City ambao walitwaa ubingwa.
Msimu wa Ligi Kuu England unatarajiwa kumalizika wikiendi ijayo, ambapo Arsenal itamaliza ugenini na Southampton.