Baada ya Mabingwa wa kihistoria wa Ulaya, Real Madrid kuiondoa Atletico Madrid katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA), sasa itakutana na Arsenal katika hatua ya robo fainali.
Real Madrid imeibuka na ushindi katika mchezo uliochezwa jana kwenye uwanja wa nyumbani wa Atletico Madrid, Riyadh Air Metropolitano.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa, ilishuhudiwa Madrid ikipata ushindi kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 120 Atletico kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kupitia bao la Conor Gallagher dakika ya kwanza ambalo lilifanya matokeo ya jumla kuwa 2-2 kufuatia mchezo wa kwanza Real Madrid kushinda 2-1.
Penalti ya ushindi kwa Real Madrid ilipigwa na beki, Antonio Rüdiger.

Julian Alvarez pamoja na Marcos Llorente waliokosa kwa upande wa Atletico huku Lucas Vázquez akikosa kwa Real Madrid.
Katika hatua ya robo fainali, Arsenal itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates, Aprili 8, 2025 huku mchezo wa marudiano ukichezwa, Santiago Bernabeu Aprili 16, 2025.
Katika hatua hiyo ya robo fainali, PSG itakutana na Aston Villa wakati Barcelona baada ya kuiondoa Benfica, sasa itakutana na Borussia Dortmund ambayo imeitoa Lille.
Bayern Munich iliyoitoa Bayer Leverkusen, itakutana na Inter Milan ambayo imeiondosha Feyenoord.