Arsenal, Man City kumaliza ubishi Emirates leo

LONDON, ENGLAND”: MANCHESTER City inasema huko kwenu Erling Haaland atakabwa na nani…Arsenal inajibu huku kwetu yupo Gabriel Magalhaes haachi kitu.

Mambo ni moto. Lakini, yanini kuandikia mate wakati wino upo?

Kila kitu kitafahamika baadaye leo huko Emirates. Beki wa mpira, Gabriel ataongoza safu ya ulinzi ya Arsenal wakati itakapoikaribisha Manchester City, itakayomtanguliza mbele straika wa mabao, Haaland katika mechi ya kibabe kabisa katika mchakamchaka wa Ligi Kuu England.

Shughuli ya Gabriel uwanjani ni pevu. Na Haaland mambo yake ni balaa. Itakuwaje?

Bato la Gabriel na Haaland ndilo litakalonogesha kipute hicho, ambacho kitakutanisha sura nyingi zinazofahamika, ikiwamo kocha Mikel Arteta na winga wake Raheem Sterling, ambao watamenyana na waajiri wao wa zamani, Man City inayoongozwa na kocha Pep Guardiola.

Beki Gabriel amefanyiwa rafu mara 11 katika mechi 10 za mwisho, wakati Haaland amefanya rafu mara saba katika mechi 11 za mwisho. Sasa wanakutana wenyewe kwa wenyewe, patanoga hapo Emirates usiku wa leo.

Kiungo na nahodha wa The Gunners, Martin Odegaard alisema Arsenal ipo tayari kwa vita kwenda jino kwa jino na wapinzani wao hao, Man City.

Supastaa huyo wa kimataifa wa Norway, Odegaard alisema upinzani baina ya Arsenal na Man City uliisaidia timu hizo kushindana mwanzo mwisho kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kwa miaka ya hivi karibuni.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Wachezaji wa Man City na Arsenal walihusika kwenye purukushani za kushikana mashati mwishoni mwa mchezo wao uliopita uliomalizika kwa sare uwanjani Etihad, Septemba mwaka jana, wakati Haaland alipofanya staili yake maarufu ya “kuweni watulivu” kitu ambacho kilionekana kuwakera upande wa pili.

Odegaard alisema: “Nadhani ni kawaida unapocheza mechi kubwa ambazo zina upinzani mkali. Unapambana na unataka kuwa bora. Hivyo ndivyo inavyokuwa na wakati mwingine moto unawaka kabisa. Hawa Man City, tumekuwa tukipambana nao kwenye mbio za ubingwa kwa miaka ya hivi karibuni na hii inatufanya tuwe bora. “Inakufanya unakuwa bora na hicho ndicho tunachotaka kukipata msimu huu. Ni ngumu kulinganisha, lakini nadhani imekuwa mechi kubwa katika miaka miwili iliyopita, hasa mwaka jana tulipambana hadi mwisho. Nadhani ni jambo la kawaida kwa kila mtu kuweka akili yake kwenye mechi, kuanzia mashabiki hadi wachezaji, hilo linaongeza zaidi joto. Inaleta hisia kali kucheza mechi kama hizi. Kila mtu anaisubiria kwa hamu.”

Katika mechi iliyopita ilimshuhudia Arteta akiingia kwenye vita na Haaland, wakati Arsenal ilipocheza na wachezaji 10 uwanjani kwa kipindi chote cha pili baada ya Leandro Trossard kutolewa kwa kadi nyekundu na Man City ilisawazisha dakika za majeruhi kufanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 2-2.

Arsenal na Man City imekuwa mechi yenye upinzani mkali kwa siku za karibuni licha ya kwamba Arteta na Guardiola walikuwa marafiki wakubwa walipokuwa pamoja kwenye benchi la ufundi huko Etihad.

Straika, Haaland atakuwa adui wa kwanza wa mashabiki wa Arsenal uwanjani Emirates leo, lakini Odegaard alifichua kwamba bado wamekuwa marafiki wakubwa na mshambuliaji huyo kwa sababu wanachezea timu moja ya taifa, ambayo ni Norway.

Odegaard alisema: “Sisi ni marafiki wazuri. Yeye na wachezaji wengine wachache kwenye timu ya taifa tumekuwa na kundi letu la kujadiliana vitu, tunawasiliana sana. Hatujazungumzia mechi, lakini ni rafiki yangu na nazungumza naye sana.”

Pointi sita zimetofautisha Arsenal na Man City kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na utamu zaidi, zinakutana leo. Itakuwaje?

Je, pengo la pointi litaongezeka na kufikia tisa au litapungua na kubaki tatu? Au kipute hicho kitafanya pengo la pointi kuwa saba? Inavutia.

Kipute hicho kinakutanisha mtu na bosi wake wa zamani, Arteta na Guardiola. Hicho ndicho kinachofanya mechi hiyo kuwa na msisimko mkubwa.

Arsenal imekusanya pointi 47 katika mechi 23, hivyo watashuka uwanjani kwao Emirates kuikaribisha Man City yenye pointi 41 kwenye mechi 23 huku zote zikipambana kuifukuzia Liverpool kileleni, ambayo jana Jumamosi ilikuwa na shughuli ya kuikabili Bournemouth.

Mechi tano zilizopita baina yao, Arsenal imeshinda moja, Man City mbili huku mbili nyingine zikimalizika kwa sare. Lakini, kwa ujumla wake kwenye rekodi zao za Ligi Kuu England, miamba hiyo imekutana mara 55, ambapo Arsenal imeshinda 24, mara 13 nyumbani na 11 ugenini, huku Man City ikiwa imeshinda 19, mara 12 nyumbani na saba ugenini. Mechi 12 zilimalizika kwa sare. Je, safari hii itakuwaje? Majibu ni leo usiku.

Kwenye Ligi Kuu England leo zitapigwa mechi za kibabe tupu. Ukiweka kando kipute hicho cha Emirates, kutachimbika wakati Brentford itakapokuwa nyumbani kucheza na Tottenham, wakati Manchester United itajimwaga Old Trafford kukipiga na Crystal Palace. Shughuli ni pevu.

Man United na Palace zimekutana mara 31 kwenye Ligi Kuu England, ambapo Mashetani Wekundu wameshinda 19, mara 11 walipocheza nyumbani na nane ugenini, huku Palace yenyewe imeshinda tano, mara tatu ilipocheza ugenini na mbili nyumbani, wakati mechi saba zilimalizika kwa sare.

Spurs itakwenda Gtech Community kuikabili Brentford huku ikiwa na rekodi tamu ambapo kwenye mechi saba ilizokutana kwenye Ligi Kuu England, tatu zilizimalizika kwa sare, huku yenyewe ikishinda tatu zote ilipocheza nyumbani na Brentford imeshinda moja tu ilipocheza ugenini. Utamu wa mechi hiyo ni kwamba Spurs haijawahi kushinda ugenini dhidi ya Brentford, wakati wenyeji hao pia hawajawahi kushinda nyumbani dhidi ya Spurs.

Balaa hilo la Ligi Kuu England litaendelea kesho Jumatatu kwa mchezo mmoja utakaopigwa huko Stamford Bridge, ambapo Chelsea itakipiga na West Ham United kwenye London derby. Hiyo itakuwa mechi ya 58 baina yao kwenye Ligi Kuu England, ambapo 57 zilizopita, Chelsea imeshinda 31, mara 18 nyumbani na 13 ugenini, huku West Ham United imeshinda 16, mara 11 ilipocheza nyumbani na tano ugenini. Mechi 10 baina yao zilimalizika kwa sare.