Arsenal, Inter Milan zatinga nusu fainali UEFA

Arsenal imefuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu katika historia ya klabu hiyo kufuatia jana kuichapa Real Madrid mabao 2-1.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, wenyeji Real Madrid walikuwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo kwani walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 waliyopoteza mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Emirates.

Bukayo Saka alikuwa wa kwanza kuiduwaza Real Madrid alipofunga bao la kuongoza dakika ya 65 akimalizia pasi ya Mikel Merino kabla ya Vinicius Junior kufunga bao la kusawazisha dakika ya 67 baada ya beki William Saliba kufanya makosa.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, Real Madrid iliendelea kufanya mashambulizi lakini Arsenal ilikaa imara huku ikifanya mashambulizi ya kushtukiza ambapo ilishuhudiwa dakika ya 90+3 Gabriel Martinelli akifunga bao la pili baada ya kuitumia vizuri pasi ya Mikel Merino na kuipa Arsenal ushindi huo.

Arsenal imekuwa timu ya kwanza kuifunga Real Madrid nje ndani katika mechi za mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya huku pia ikishinda mara mbili kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu. Awali ilikuwa mwaka 2006 kwa kuifunga bao 1-0.

Kwa ushindi huo, Arsenal imetinga nusu fainali kwa jumla ya mabao 5-1 huku ikienda kukutana na PSG Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Emirates wakati mechi ya marudiano itachezwa Mei 7 kwenye Uwanja wa Parc des Princes, Ufaransa.

Mchezo mwingine ulichezwa Italia kwenye Uwanja wa San Siro ambapo ilishuhudiwa wenyeji Inter Milan wakitinga nusu fainali baada ya kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bayern Munich.

Inter Milan imefanikiwa kusonga kwa jumla ya mabao 4-3 kwani mchezo wa kwanza ilipokuwa ugenini ilipata ushindi wa mabao 2-1.

Katika hatua ya nusu fainali, Aprili 30 mwaka huu Inter Milan itaifuata Barcelona, kisha itakuwa nyumbani Mei 6 katika mchezo wa marudiano.

Mchezo wa fainali ya michuano hiyo umepangwa kuchezwa Mei 31 mwaka huu, Allianz Arena nchini Ujerumani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *