
Arsenal inapambana kuchukua taji hili kwa mara ya kwanza katika historia yao ingawa hapo awali iliwahi kushinda lakini wakati huo lilikuwa linaitwa European Cup Winners msimu wa 1993-94.
Kwa upande wa Madrid, hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kutolewa katika hatua ya robo fainali baada ya kufika hatua hiyo, mara ya mwisho ilikuwa msimu wa 2003/04.
REKODI ZILIZOWEKWA
Arsenal imeweka rekodi ya kumwondoa bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya pili katika historia yao, mara ya kwanza ikiwa dhidi ya AC Milan msimu wa 2007-08.
Katika mchezo wao dhidi ya Madrid, kiungo wa Gunners, Mikel Merino ambaye alitoa asisti mbili aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili wa timu ya ugenini kutoa asisti mbili katika mechi ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, baada ya Dusan Tadic wa Ajax mnamo Machi 2019.
Arsenal pia ndio timu ya kwanza kabisa kushinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Real Madrid kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kwa mashindano yote.
Tangu kuanza kwa msimu uliopita, Harry Kane amehusika moja kwa moja katika mabao mengi zaidi 101, kuliko mchezaji yeyote katika ligi tano bora barani Ulaya katika mashindano yote.
Thomas Muller alicheza mechi yake ya 163 ya Ligi ya Mabingwa usiku Jumatano, akifikia idadi ya mechi za Lionel Messi.
Katika historia ya mashindano haya, ni Cristiano Ronaldo (183) na Iker Casillas (177) tu ndio waliocheza mechi nyingi zaidi.
Jude Bellingham alicheza mechi yake ya 47 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano na akaifikia rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 21 au chini ya hapo katika historia ya mashindano, mchezaji aliyekuwa anashikilia rekodi hiyo ni Iker Casillas ambaye akiwa na umri kama huo alishacheza mechi 47.
Myles-Lewis Skelly ni mmoja kati ya wachezaji watatu wenye umri wa miaka 18 kuanza mechi ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ugenini dhidi ya Real Madrid, wengine waliowahi kufanya hivyo ni Cesc Fabregas (Februari 2006, Arsenal) na Max Meyer (Machi 2014, FC Schalke 04).